Frank Aman – Geita.
Jeshi la Polisi Mkoani Geita linafanya uchunguzi wa ajali iliyosababisha vifo vya watu watatu, mwanaume, mwanamke na mtoto aliyekuwa mgongoni ambao bado hawajatambuliwa na inadaiwa ni wa familia moja waliohamia hivi karibuni katika eneo hilo.
Ajali hiyo imetokea Aprili 2, 2025 majira ya saa 2 usiku katika Kijiji cha Nyabilele, kilichopo Kata ya Mganza katika barabara itokayo Mganza kwenda Chato.

Inaarifiwa kuwa, Dereva aliyekuwa akiendesha gari hiyo ambaye hakufahamika alikimbia mara baada ya ajali kutokea na Miili ya marehemu imehifadhiwa Kituo cha Afya Muganza – Chato kwa taratibu za uchunguzi na utambuzi.
Aidha, Jeshi la Polisi pia linamshikilia mtu mmoja, Abel Josephat (43), Mkazi wa Bwawani Nyamirembe Wilaya ya Chato, kwa tuhuma ya kupiga picha miili ya waliofariki katika ajali hiyo na kuzisambaza kwenye mtandao wa kijamii zikiwa na maudhui yasiyokubalika kisheria.