Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Polisi watatu mbaroni kwa madai ya wizi wa mil. 90

Maafisa watatu wa Jeshi la Polisi wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za unyang’anyi wa kutumia silaha na kuiba Sh. milioni 90.

Washtakiwa hao ni Koplo Ramadhani (42) maarufu Rasta, Koplo Majid Abdallah (35) na Koplo Stella Mashaka (40).

Wakili wa Serikali, Neema Moshi, aliwasomea washtakiwa hao shtaka moja la unyang’anyi linalowakabili, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi.

Alidai washtakiwa kwa pamoja Agosti 28, mwaka huu, maeneo ya Kurasini, jirani na Ofisi ya Uhamiaji, wilayani Temeke, waliiba Sh. milioni 90.

Wakili Neema alidai washtakiwa kabla na baada ya kuiba fedha hizo, walimtishia kwa bunduki Grace Matage kwa nia ya kujipatia fedha hizo.

Baada ya kusomewa mashtaka washtakiwa wote walikana kutenda makosa hayo, upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba kesi iahirishwe hadi tarehe nyingine.

Upande wa washtakiwa haukuwa na pingamizi, mahakama iliahirisha shauri hilo hadi Novemba 13, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Msumi aliamuru washtakiwa warudishwe rumande hadi tarehe hiyo kwa sababu shtaka linalowakabili halina dhamana

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *