Jeshi la polisi Mkoani Manyara limekanusha Taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria ,Pauline Gekul alikamatwa mpakani akitoroka kuelekea nchini Kenya, na kusema kuwa hakukamatwa ila alitumiwa wito kwa ajili ya mahojiano.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara ACP George Katabazi amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tuhumu zinazomkabili kiongozi huyo,na kuongeza kuwa yuko nje kwa dhamana, na kuwataka wananchi kuwa na subira na kuliacha jeshi la polisi lifanye kazi yake.
Gekul anatuhumiwa kutoa maelekezo kwa kundi la vijana wake kumwingizia chupa sehemu ya haja kubwa mfanyakazi wake, Hashim Ally au kumpiga risasi kwa madai kwamba alitumwa kimkakati kwenda kwenye hoteli yake ya Paleii Lake View Garden inayomilikiwa na mbunge huyo.
Jana jumapili Novemba 26,2023 Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara kilifanya kikao kujadili sakata la Mbunge huyo, ambapo mwenyekiti wa CCM mkoa wa Manyara, Peter Toima aliahidi kutoa maelezo kamili leo Novemba 27 2023.