POLISI MWANZA WAFANYA UKAGUZI WA KUSHTUKIZA KWA MABASI YA ABIRIA.

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza katika kudhibiti ajali za Barabarani limefanya zoezi la ukaguzi wa kushtukiza leo Disemba 27.2024 katika eneo la Usagara kwa magari yanayobeba abiria wanaokwenda mikoani ili kuona namna madereva wa magari hayo wanavyofuata sheria za usalama barabarani.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Mwanza, Sunday Ibrahim amesema zoezi la ukaguzi huo litakua zoezi endelevu na amewakumbusha abiria wanaopanda magari hayo kutambua haki zao za msingi huku pia akiwataka kutofumbia macho  vitendo viovu vinavyofanywa  na baadhi ya madereva na jambo hilo linawezekana endapo watatoa taarifa kwa jeshi la Polisi pale vitendo hivyo vinapojitokea.

Katika ukaguzi huo magari mawili yamekamatwa na wamiliki kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kushindwa kutimiza masharti/kanuni inayowataka kuajiri madereva wawili kwa mabasi yanayosafiri umbali mrefu wa zaidi ya masaa nane.

Kwa upande wao baadhi ya abiria wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa kufanya ukaguzi wa kushitukiza na kuomba liwe endelevu kwani imebainika kuwa baadhi ya madereva wamekuwa wanafata sheria za usalama barabarani pale wanapowaona askari kitendo ambacho kinahatarisha maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara.

“Zoezi linalofanywa na Jeshi la Polisi ni kwaajili ya usalama wetu sisi wananchi, sio vyema gari la mwendo mrefu likawa na dereva mmoja” amesema Donald Chakachaka (abiria)

“Nimelipokea zoezi hili kwa mikono miwili kwasababu linatusaidia sisi wasafiri kutuepusha na ajali kwahiyo nawapongeza Polisi wako sawa” amesema Mwajima Hamis (abiria)

Naye, dereva wa kampuni ya mabasi Nyehunge Hassan Maneno amesema kwa sasa vitendo vya uvunjaji wa sheria za usalama barabarani vimepungua kwa mkoa wa Mwanza.

“Hakuna zile vurungu za kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari , tunazingatia mistali sana sana kwa hiyo nalipongeza sana jeshi la polisi kwa kazi nzuri wanayofanya ” amesema Maneno.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *