Na Daniel Gahu – Katavi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, kupitia Kitengo cha Polisi Jamii, limeitembelea Shule ya Msingi Kakuni, Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, shule aliyowahi kusoma Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda, na kutoa msaada mbalimbali kwa wanafunzi pamoja na kuchangia ujenzi wa madawati.
Katika ziara hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, SACP Kaster Christian Ngonyani, alitoa fedha taslimu zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 1.2, ambazo zitatumika katika kugharamia bima za afya kwa wanafunzi 12 pamoja na kutengeneza madawati kwa ajili ya shule hiyo.

Kati ya fedha hizo, kiasi cha Shilingi 100,800 kimetengwa kwa ajili ya bima za afya za wanafunzi 12, huku fedha iliyobaki, ambayo ni zaidi ya Shilingi milioni moja, ikielekezwa katika utengenezaji wa madawati.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kamanda Ngonyani aliwahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kuzingatia elimu kama msingi wa kutimiza ndoto zao za baadaye.

Alisema wanafunzi wanapaswa kujifunza kutoka kwa viongozi waliofanikiwa, akitolea mfano wa Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda, ambaye alianza safari yake ya kielimu katika shule hiyo kabla ya kufikia nafasi ya juu ya uongozi nchini.
Kamanda Ngonyani pia aliwakumbusha wanafunzi kuepuka vitendo vinavyokiuka maadili na kuharibu mustakabali wao, akiwataka kuwa na nidhamu na kujenga tabia njema zitakazowasaidia kufikia malengo yao.

Mbali na mchango wa fedha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi liliwapatia wanafunzi mahitaji mbalimbali kama sehemu ya kuimarisha uhusiano na jamii pamoja na kuwapa motisha ya kusoma.
Miongoni mwa vitu vilivyotolewa ni mchele, unga, madaftari na kalamu za kuandikia.
Aidha, Kamanda Ngonyani ametoa fedha kwa ajili ya kununua sare za shule kwa wanafunzi ambao sare zao zimechakaa na hivyo kuwasaidia kuendelea na masomo katika mazingira bora.

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Katavi, John Mwaipungu, aliwahimiza wanafunzi kuongeza bidii katika masomo ili kutimiza ndoto zao na kuwa viongozi wa baadaye.
Mwaipungu pia aliwataka wanafunzi kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya vitendo viovu katika jamii kwa kutoa taarifa kuhusu matukio wanayoyaona au kuyafahamu yanayoweza kuhatarisha usalama na ustawi wa watoto.

Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi katika kuimarisha ushirikiano kati ya Polisi na jamii, huku ikilenga pia kuhamasisha wanafunzi kuthamini elimu, nidhamu na maadili mema.
Shule ya Msingi Kakuni ina historia ya kipekee kwa kuwa ni miongoni mwa shule zilizotoa msingi wa elimu kwa Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda, ambaye baadaye alifikia nafasi ya juu katika uongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


