Wazazi na walezi wa wanafunzi mkoani Mwanza wamelalamikia suala la uwepo wa michezo ya mitandaoni maarufu kama play station inayochezwa katika sehemu mbalimbali ya mkoa huo na kudai kuwa ndio chanzo cha utoro wa watoto shuleni huku pia kikitajwa kuwa chanzo cha uhalifu ndani ya mkoa huo.

Wakizungumza na Jambo Fm kwa nyakati tofauti wazazi hao wamesema baadhi ya watoto wamekuwa wakitoroka shule kwa ajili ya kwenda kucheza michezo hiyo na kwa kiasi kikubwa imekua ikiathiri maendeleo ya wanafunzi hao kwani wamekua wakitumia muda mwingi kwenye michezo hiyo huku wakishindwa kufanya masuala ya msingi yanayohusu masomo yao.
Akizungumzia michezo hiyo kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa amesema ni wajibu wa viongozi wa mtaa kuhakikisha wanatoa taarifa kwa jeshi la polisi pale wanapoona michezo hiyo inahatarisha usalama wa wananchi huku pia akiwataka watoe taarifa kwa viongozi wa halmashauri ili mashine hizo ziweze kuondolewa katika maeneo ambayo ni hatarishi kwa wanafunzi hao.
Mutafungwa amewataka wazazi na walezi wa mkoa wa Mwanza kuhakikisha wanawalea watoto katika maadili yanayofaa ili waweze kuondokana na masuala ya uhalifu pamoja na masuala mengine ambayo yanaweza kuhatarisha salama wao.