Na Saada Almasi, Meatu – Simiyu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Anthony Philipo, ametoa maagizo ya dharura kwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), kuhakikisha ukarabati wa mara kwa mara unafanyika katika maeneo yaliyoathirika na mvua kubwa zinaendelea katika maeneo mengi nchini ikiwemo wilaya ya Meatu zilizosababisha kukatika kwa mawasiliano.
Akitoa majumuisho kabla ya kufunga kikao cha Baraza la madiwani la halmashauri hiyo lililokuwa likiwasilisha taarifa za kata 29 zinazounda wilaya hiyo, Philipo amesema kwamba mawasiliano ya barabara ni nguzo ya msingi ya uchumi na ustawi wa wananchi, na kwamba hakuna sababu ya kuvumiliana na hali inayoweza kusababisha wananchi kukosa huduma hasa ukizingatia mabadiliko ya tabia nchi yameleta mvua zaidi ya kiwango.

“Nitoe maelekezo kwa kuwa meneja wa TARURA Meatu upo hapa jaribuni kuangalia upya hizi barabara ambazo zinawapa gharama kubwa wananchi baada ya kukatika kwa sababu wanatumia pesa zaidi kutoka eneo moja hadi lingine na wengine kukwama kabisa kufanya shughuli zao kwa kukosa mawasiliano kutoka mahapa pamoja kwenda kwingine,” amesema Anthony.
“Nitoe mfano tu barabara inayounganisha kata ya Mwangudo kwenda Mwanhuzi ilipata shida watu walilazimika kutoka Makao hadoi mjini kwa shilingi elfu 60 na ukizingatia kupanda kwa bei ya mafuta mtu anakuwa hana jinsi,atalipa kumbe ilikuwa ndiyo faida yake ya biashara anayofanya hebu fikiria ameathirika namna gani?sasa niwaombe tena kuna fungu la serikali lakini hata mafungu ya dharura tumieni kutatua changamoto hizi kwa wananchi wetu,” ameongeza Anthony.

Sambamba na hilo Anthony pia ameelekeza zahanati ambazo tayari zimekamilika kuanza kazi ili wananchi waendelee kupata huduma na ambazo bado hazina vifaa tiba vya kutosha ziweze kupelekewa ili kuwapunguzia mwendo wa kufuata huduma maeneo mengine
Changamoto hiyo, ambayo imetajwa na zaidi ya nusu ya Madiwani waliohudhuria kikao hicho, pia ukosefu wa matundu ya vyoo katika baadhi ya shule ikiwemo shule ya Msingi Muungano iliyopo kata ya Mwandoya jimbo la Kisesa ikachukua sura mpya ya kutokuwa na uwiano sawa na idadi ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo.

“Shule ya Muungano ambayo ina wanafunzi 1400 ina matundu 4 ya vyoo ukiangalia kwa uwiano huu ni changamoto kubwa kwa watoto wetu na hatari maana yatakapoingia magonjwa ya mlipuko itakuwa hatari kubwa, lakini pia madarasa hayatoshi mwakani tunategemea madarasa mawili,”
“Yaani darasa la sita na darasa la saba kumaliza elimu ya msingi changamoto ni kuwa madarasa yaliyopo hayatoshi tunawezaje kuwafundisha watoto kufaulu maana idadi ya madarasa yaliyopo ni 8 huku uhitaji ukiwa ni madarasa 31?,” alisema Diwani wa Kata ya Mwandoya, Daniel Salu Nsogotelwa.

Pamoja na changamoto hizo baraza hilo pia lilipokea taarifa za baadhi ya madaraja ambayo baadhi ya wakandarasi walipokea tenda na kutengeneza chini ya viwango hali iliyosababisha wananchi kuendelea kupata adha baada ya kukatika muda mfupi baada ya kutengenezwa likiwepo daraja katika kata ya Mwasengela jimbo la Kisesa.


