Na Cecilia Shiratu, Bukoba – Kagera.
Wakulima Wadogo wapatao 2,193 mkoani Kagera, wanatarajiwa kunufaika na pampu 175 za umwagiliaji zenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 zilizotolewa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, katika juhudi za kuongeza tija na kuimarisha uzalishaji wa mazao kwa njia ya umwagiliaji.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Ramadhani Kido, alisema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuendeleza sekta ya kilimo, ikiwemo kuwezesha vikundi vya wakulima wadogo, vijana na wanawake wanaojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji kupata uhakika wa maji na kuongeza uzalishaji.

Alisema Mkoa wa Kagera umepokea pampu hizo 175 ambazo zitasambazwa katika halmashauri nane za mkoa huo, huku zikitumika katika miradi mbalimbali ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji na kuwasaidia wakulima kuondokana na utegemezi wa mvua pekee.
RC Kido aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwezesha upatikanaji wa pampu hizo akisema, ni uwekezaji muhimu unaolenga kubadilisha mfumo wa uzalishaji wa mazao kutoka kilimo kinachotegemea mvua hadi kilimo chenye tija na uhakika wa uzalishaji katika misimu zaidi ya mmoja kwa mwaka.

“Pampu hizi zitawawezesha wakulima kupata uhakika wa maji kwa ajili ya kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao, hatua ambayo itasaidia kuboresha kipato cha wananchi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa,” alisema RC Kido.
Mhandisi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji mkoani Kagera, Said Mbiru, amesema mkoa huo una takribani hekta 90,000 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini kwa sasa ni hekta 23,000 pekee ndizo zinazoendelezwa.

Alisema kupitia hatua ya kuongezwa kwa hekta 1,117 katika eneo la umwagiliaji, eneo linalolimwa kwa mfumo huo linatarajiwa kufikia jumla ya hekta 24,117.
Mbiru alisema pampu hizo zina uwezo wa kutoa maji kwa kiwango cha lita 80 kwa saa na kuwezesha kumwagilia hekari 28 kwa saa 1, hivyo kusaidia kuongeza upatikanaji wa maji katika maeneo ya kilimo na kuimarisha uzalishaji wa mazao.




