Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Mfuko wa Hifadhi ya jamii (NSSF) mkoa wa Shinyanga, umezindua wiki ya huduma kwa wateja huku kauli mbiu kwa mwaka 2025 ikisema “KIDIGITAL TUMEWEZA” katika ofisi za NSSF mkoa wa Shinyanga.
Katuka uzinduzi huo, Meneja wa NSSF Mkoa, Amina Mdabi amewataka wanachama wa mfuko huo, kwenda kuwa mabalozi kwa wengine, ili wajiunge nao kwani umekuwa na faida nyingi.

Amesema, kwa kujiunga na mfuko huo jamii itapata faida katika maisha ya baadaye, kwani huduma za NSSF kwasasa zimeboreshwa kidijitali kwa mwanachama kupata huduma mbalimbali akiwa katika eneo lake popote alipo
Aidha, Amina amesema wamekuwa wakiwahudumia Wastaafu katika sekta zote kwa weledi kwa kuhakikisha fedha zao za mafao wanazopata kila mwezi zinatoka kwa wakati.

“Napenda kuwasihi sana wazee wangu ambao mmekuwa mkipokea pensheni mkawe mabalozi wetu katika jamii ili wajiunge na mfuko wetu kwa kuwaptia elimu juu ya faida mnazopata kupitia mfuko wa NSSF,“ amesema Amina.
Naye Mkuu wa Idara ya Matekelezo wa NSSF mkoa wa Shinyanga, Hawa Godigodi amesema kuimarishwa kwa huduma za mfuko huo kumepelekea mwanachama kufahamu taarifa zake kwa urahisi tofauti na kipindi cha nyuma.

Aidha, amewataka waajiri katika mashirika, makampuni na watu binafsi kuwachangia wafanyakazi wao, ili waweze kunufaika na huduma za NSSF.
Nao baadhi ya Wastaafu na Wanachama wa mfuko huo, wameishukuru NSSF kwa kuwalea vizuri na kuwapa fedha zao za kila mwezi kwa wakati, huku wakizisihi baadhi ya Taasisi na watu binafsi ambao bado hawajajiunga na mfuko kuchangamkia fursa.


