Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Mgombea Udiwani Kata ya Ngokolo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jackline Isaro amewahidi Wananchi wa Kata hiyo, kuendelea kuleta maendeleo zaidi endapo watampatia ridhaa ya kuwaongoza ikiwa ni pamoja kusikiliza kero za Wananchi katika mitaa yote inayounda kata hiyo.
Jackline ameyabainisha hayo kwenye Mkutano wa Kampeni uliofanyika Mtaa wa Mwinamila Kata ya Ngokolo, ikiwa ni muendelezo wa kupita mtaa kwa mtaa kuomba kura kwa Wananchi, ili waweze kumchagua kuwaongoza.
Amesema, Kiongozi anayewafikia watu na kujua changamoto zao ndiye anaweza kuleta maendeleo kwa haraka kuliko yule anayependa kukaa Ofisini, hivyo Kata ya Ngokolo itegemee maendeleo kwa kasi akianzia pale alipoishia mtangulizi, Victor Mkwizu

“Mkinipatia ridhaa ya kuwa Diwani wenu Oktoba 29, sitakuwa kiongozi wa kukaa ndani, nitashirikiana na viongozi wa serikali za mtaa kufanya mikutano ya hadhara kila baada ya miezi mitatu kusikiliza kero zenu na kuzipatia ufumbuzi na hatimaye kuwaletea maendeleo,“ amesema Jackline.
Ameongeza kuwa anazifahamu changamoto zinazowakabili Wafanyabishara wa soko la mitumbani lililopo katika kata hiyo na kwamba atazifanyia kazi, ili waweze kufanya kazi utulivu na kuendelea kuimarisha uchumi wao.

Akizungumzia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, Jackline aliwahidi Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu katika Kata hiyo kuwa, atakapopata ridhaa ya kuwa diwani atapambana ili kuhakikisha wanaipata na kuinuka kiuchumi.
Aidha, amewaomba pia wananchi siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kuwachagua wagombea wote wanaotokana na CCM na kwamba wasikubali kushawishiwa kufanya maandamano yasiyo na tija, ambayo yatavuruga amani ya nchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Anold Makombe amewaomba Wananchi wa Ngokolo waendelee kuiamini CCM na kuwapa ridhaa ya miaka mitano ya kuongoza, ili waendelee kuwaletea maendeleo kwani ni chama chenye sera na ilani nzuri inayogusa maslahi ya Wananchi.


