
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Aikael Mbowe ametangaza rasmi kuwa atagombea kwa mara nyingine Uchaguzi wa Chama hicho ili kutetea kiti chake cha Uenyekiti wa CHADEMA Taifa akichuana na Tundu Lissu na Viongozi wengine watakaojitokeza kugombea nafasi hiyo.
Mbele ya Wahariri na Waandishi wa Habari leo Disemba 21,2024, Mbowe amesema “Nimetafakari kwa kina sana, nimesema mara nyingi nilitamani kuondoka lakini siwezi kuondoka na minyukano ambayo ipo ndani ya Chama , kwahiyo CHADEMA nipo, nitakuwepo, nitagombea na Mimi na Viongozi wenzangu wanaoniunga mkono na wasioniunga mkono naamini tutakutana kwenye mazungumzo tuweke mambo sawa, sijawahi kuzuia Watu kugombea, anayetaka kugombea tukutane kwenye box” – Mbowe
“Nilipokea kijiti cha kuongoza Chama chetu September 14,2004, katika miaka hiyo 20 ni kipindi cha miaka 11 tu ya kwanza ambapo tulifanya kazi kikamilifu ya kujitoa ili kukijenga Chama chetu kuwa Chama makini na tukapiga mafanikio ya kufanya tuwe Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania” – Mbowe

Mara baada ya kukamilisha mazungumzo na Wahariri pamoja na Waandishi wa habari, Mwenyekiti Mbowe alielekea Mikocheni yaliko Makao Makuu ya CHADEMA kwa ajili ya kuchukua fomu za kugombea Uenyekiti tena.