Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu ameiambia Mahakama kuwa hajahukumiwa hukumu ya kifo lakini amewekwa eneo maalum kinyume cha sheria na haki zake za msingi zinapuuzwa, ikiwemo kuabudu na kufanya mazoezi.
Lissu ameyasema hayo hii leo Juni 16, 2025 mbele ya Mahakama ya Kisutu Jijini Dar es Salaam na kudai kuwa eneo hilo maalum alilowekwa ni la watu wanaosubiri kunyongwa.
Amesema, “Gereza la Ukonga kuna sehemu moja inaitwa ‘special room’ eneo maalum ambalo wanakaa wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kifo kwa kunyongwa, mimi ninakaa hiyo sehemu wanayokaa wanaosubiri kunyongwa.”

“Ukiwa death rock maana yake ni nini? Kanuni ya 33 inazungumzia watu walio death rock inasema hivi ukikaa death rock Mheshimwa kama ninachokaa mimi wakati sijahukumiwa kifo angalau bado sheria inasema wale waliohukumiwa kifo wanatakiwa watenganishwe na wafungwa wengine,” alifafanua Lissu.
Aliongeza kuwa, “mimi nimekaa death rock tangu ljumaa Kuu mpaka leo na nikitoka kuonana na mawakili wangu au ndugu zangu naambatana na Askari wawili muda wote kama inavyotakiwa kwa waliohukumiwa kifo.”
Baadaye, upande wa Jamhuri ulidai haujapewa nafasi ya kusikilizwa kutokana na madai hayo, ambapo Hakimu Kiswaga alisema yamebainishwa na Mshtakiwa kama taarifa, hivyo yafanyiwa kazi.


