‘NIMERIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE WA SHINYANGA’ – NAIBU WAZIRI KASEKENYA..

NA EUNICE KANUMBA- SHINYANGA.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, leo tarehe  18 December 2024  amekagua maendeleo ya upanuzi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga uliopo kata ya  Ibadakuli,  Manispaa ya Shinyanga, na kuagiza  ujenzi  huo ukamilike kwa wakati ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa mkoa huo na mikoa jirani.

Mhandisi Kasekenya amesema ameridhika na kasi ya ujenzi, na kusisitiza kwamba inapaswa kuendelea kwa kasi kubwa Zaidi kabla ya msimu wa mvua kuchanganya  ili mradi  huo ukamilike huo kwa wakati Aprili 1, 2025 kama ilivyokusudiwa.

“Nimeridhika na maendeleo ya ujenzi wa mradi huu, hivyo niombe kasi ya ujenzi huu iendelee ili kufikia tarehe 1, Aprili 2025, Ujenzi uwe umekamilika. Tutamuomba Mheshimiwa Rais Samia aje kutuzindulia uwanja huu ili uanze kutoa huduma kwa wakazi wa Mkoa wa Shinyanga na mikoa jirani”. amesema Mhandisi Kasekenya.

Aidha, Naibu Waziri Kasekenya ametoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za mradi wa Ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Shinyanga, unaojengwa na Mkandarasi China Hennan International Corperation Group Co. Ltd (CHICO) kwa gharama ya shilingi 49,179,439,633.00/= pamoja na VAT na ukisimamiwa na Wakandarasi kutoka Kampuni ya SMEC International ya nchini Australia kwa gharama ya Dola za Marekani 2,602,343 na Shilingi 23,735,554/= pamoja na VAT.

Amesisitiza kuwa uwanja huo utakapokamilika utakuwa ni chachu ya maendeleo na kukuza uchumi mkoani Shinyanga, Naye Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Fred Kipamila ambaye anasimamia mradi huo ameeleza kwamba ujenzi wa uwanja  huo umefikia kiwango kizuri, ambapo barabara ya  kurukia ndege (Runway) tayari imekamilika.

Aidha Mhandisi mshauri wa mradi  huo Gosberi Ruburi, amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa atasimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo ili ujenzi ukamilike kwa wakati na ndani ya muda wa mkataba, huku akiongeza kwamba serikali tayari imekwisha lipa fedha zote za mradi huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *