Na Daniel Gahu – Katavi.
Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Said Juma Mshana, leo amewasili Mkoani Katavi kwa ziara ya kikazi inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya Tanzania na DRC.
Mara baada ya kuwasili, amepokelewa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Florence Chrisant, akishirikiana na wataalamu kutoka Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja na Idara ya Uchumi na Uzalishaji.

Akizungumza mara baada ya kuwasili, Mshana amesema ziara yake inalenga kutembelea Bandari ya Karema ili kujionea namna inavyofanya kazi na mchango wake katika kurahisisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani.
“Nimekuja kujionea kwa vitendo utendaji wa Bandari ya Karema, uwezo wake katika kuhudumia mizigo, na nafasi yake katika kuimarisha biashara kati ya Tanzania na DRC pamoja na nchi nyingine za ukanda huu,” amesema Balozi Mshana.

Aidha, ameongeza kuwa katika ziara hiyo amepata fursa ya kutembelea na kukagua miundombinu ya barabara inayounganisha bandari hiyo na maeneo mengine ya kimkakati, kwa lengo la kutathmini namna inavyoweza kuimarishwa zaidi ili kusaidia ukuaji wa biashara na uchumi.
Serikali inatazamia kupunguza msongamano katika mpaka wa Tunduma kwa kuimarisha na kuhamasisha matumizi ya njia mbadala za usafirishaji wa mizigo, hususan kupitia Bandari ya Karema, hatua itakayorahisisha biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) pamoja na nchi nyingine za Ukanda wa Maziwa Makuu.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Florence Chrisant, amemkaribisha balozi huyo na kumueleza kuwa Mkoa wa Katavi una fursa lukuki za uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, biashara, kilimo na usafirishaji.
Amesema Bandari ya Karema ni miongoni mwa miundombinu yenye ubora na nafasi ya kimkakati katika ukanda wa Ziwa Tanganyika, na kwamba maboresho yanayoendelea yataifanya kuwa kichocheo kikubwa cha biashara ya kikanda.


