Na Gideon Gregory – Dodoma.
Serikali imeyatakia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kote nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji na uzalendo, ili kuimarisha utawala bora na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Hayo yameelezwa leo Agosti 13, 2025 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima wakati alipomwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Philip Isdori Mpango katika kilele cha Kongamano la Mwaka la NGOs Jijini Dodoma
Gwajima amesisitiza kuwa mashirika hayo lazima yaendelee kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi sambamba na vipaumbele vya kitaifa.

Aidha, amezindua Mwongozo wa Uzingatiaji wa Uwazi wa Masuala ya Kifedha na Ushirikiano kati ya Serikali na Asasi Zisizo za Serikali, pamoja na Kamati ya Kitaifa ya Mchakato wa Uanzishwaji wa Mfuko wa Pamoja wa Ruzuku kwa NGOs (NBF).
Amesema mfuko huo utasaidia mashirika kupata ufadhili bila masharti magumu na kuongeza uhimilivu wa miradi yao.
Pia amewataka viongozi wa NGOs kutumia fursa ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano kuendeleza mchango wao katika sekta za afya, elimu, kilimo, maji, mazingira na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2025, NGOs zilizopewa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura na uangalizi wa uchaguzi zimetakiwa kufanya kazi kwa weledi na kuhamasisha wananchi kushiriki kwa amani na utulivu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali Jasper Makala amesema changamoto kubwa inayowakabili ni malimbikizo ya madeni ya kodi kwenye mfumo wa kielektroniki wa TRA.
“Kama ambavyo tulielekezwa katika jukwaa la mwaka 2023 na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, tumeweza kuwasilisha mapendekezo yetu kuhusu utekelezaji wa sheria za kodi kwa uongozi wa mamlaka za juu za TRA, pia baraza limewasilisha mapendekezo ya madiliko ya kodi kwa tume ya Rais ya kuthamini na kushauri kuhusu masuala ya kodi,” amesema.

Amesema ni matumaini yao kuwa mapendekezo hayo yatapewa kipaumbele na kufanyiwa kazi na mamlaka husika.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Bi. Hajjat Mwantumu Mahiza, amewaomba wanasekta hiyo kuendeleza mashirikiano kwaajili ya faida ya taifa na kizazi kijacho.
“Ndugu zangu hii nchi tinaijenga sote na kila mmoja ana dhamira njema kwa nchi yake, ni wasihi sana kila mmoja kwenye nafasi aliyopo kila unalolifanya tanguliza maslahi ya nchi kwanza, Tanzania hii ni yetu sote na inatutegemea na tunahitaji kuijenga Tanzania iwe mahali salama na penye neema nyingi kuliko tulivyoikuta sisi,” amesema.

Katika kongamano hilo, Serikali ilipongeza mashirika kwa mchango wao katika kutoa ajira, kuboresha huduma za kijamii na kushirikiana katika mchakato wa maboresho ya sheria, sera na miongozo ya sekta hiyo.


