Na Tryphone Odace, Kasulu - Kigoma.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma, limezitaka Shule za Sekondari zenye Wanafunzi wanaoishi bweni kuboresha mifumo ya umeme pamoja na kuhakikisha zina vifaa vya kutosha vya kuzimia moto, ili kuzuia na kukabiliana na majanga ya moto yanapotokea.
Akizungumza na walimu wa Shule za Sekondari Bogwe na Mwilanvya wakati wa mafunzo ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto katika shule za bweni, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kasulu, Mrakibu Msaidizi Antony Marwa, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea walimu uelewa na uwezo wa kuchukua hatua sahihi wakati wa majanga ya moto.
Amesema shule za bweni zinapaswa kuhakikisha mifumo ya umeme inakaguliwa na kuboreshwa mara kwa mara, ili kuzuia hitilafu za umeme zinazoweza kusababisha moto.

Marwa pia amesisitiza umuhimu wa shule kuhakikisha mabweni yana vifaa vya kuzimia moto vinavyokidhi mahitaji, pamoja na walimu na watumishi kuwa na ujuzi wa namna ya kuvitumia.
“Niwaombe tutoe taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kabla ya kuanza ujenzi wa mabweni, ili kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu na hatua muhimu za kuzingatia katika ujenzi” amesema Marwa.
Amesema miongoni mwa mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni uwekaji wa milango ya dharura, ambayo itasaidia kurahisisha uokoaji wa wanafunzi na watumishi pindi moto unapotokea.

Baadhi ya walimu wa Shule ya Sekondari Bogwe wamesema mafunzo hayo yamewasaidia kuongeza uelewa na ujuzi wa kukabiliana na majanga ya moto.
Wamesema elimu waliyoipata itawasaidia kuchukua hatua za haraka na sahihi wakati wa dharura, hususan katika kuwalinda wanafunzi pamoja na mali za shule.
Discussion
Reader comments
0 contributions