Na Saulo Stephen, Mbulu - Manyara.
Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Dkt. Emanuel Nuwas, ameendelea na ziara yake ya kikazi ya kutembelea vijiji mbalimbali kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kutoa mrejesho wa utekelezaji wa shughuli za Serikali.
Katika ziara iliyofanyika Julai 21, 2026 katika Kata ya Eshkesh, Dkt. Nuwas alitembelea vijiji vya Endagulda, Eshkesh na Domanga, ambapo aliwaeleza wananchi kuhusu Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027 yenye thamani ya Sh trilioni 62.3 na namna itakavyochochea maendeleo katika sekta mbalimbali.
Alisema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ya maji, barabara na umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), huku akibainisha kuwa vitongoji vitatu vya Kata ya Eshkesh tayari vimepata huduma ya umeme.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi mbalimbali, Dkt. Nuwas alisema ukarabati wa barabara ya Yaeda Chini–Nyamusta–Haydom umeanza, huku akiahidi kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji katika Kituo cha Afya Eshkesh pamoja na shule za msingi na sekondari zilizopo katika eneo hilo.
Mbunge huyo pia alipokea changamoto ya upatikanaji wa maji katika Shule za Msingi Endagulda na Domanga, ambapo aliahidi kutuma wataalamu kutoka RUWASA kufanya tathmini ya visima viwili ili kubaini uwezekano wa kuvuta maji kwa ajili ya shule hizo na wananchi wa maeneo husika.
Aidha, aliahidi kupeleka madawati 45 katika Shule ya Msingi Endagulda ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Katika sekta ya mifugo, Dkt. Nuwas aliahidi kujenga majosho mawili katika vijiji vya Endagulda na Domanga pamoja na kukamilisha ujenzi wa josho la Eshkesh, hatua inayolenga kupunguza magonjwa ya kupe na kuboresha afya ya mifugo.

Mbali na kutoa ahadi hizo, Mbunge huyo alitoa elimu kuhusu ufugaji wa kisasa na kuwahimiza wafugaji kuachana na mfumo wa ufugaji wa kizamani ili kuongeza tija na kuinua uchumi wa kaya.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa kusikiliza na kupokea kero mbalimbali za wananchi zikiwemo changamoto za mtandao wa simu, ubovu wa barabara, upatikanaji wa huduma za maji pamoja na elimu, huku Dkt. Nuwas akiahidi kuzifuatilia na kuzitafutia ufumbuzi kupitia mamlaka zinazohusika.
Discussion
Reader comments
0 contributions