Serikali ya Zambia imetangaza hali ya dharura kufuatia uhaba wa mafuta nchini humo, huku ikuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kusimamisha ushuru wa bidhaa (excise duty) kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa muda wa miezi mitatu, kuanzia Aprili 1, 2026.
Kikao maalumu cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais wa nchi hiyo, Haikande Hichilema kilifikia maamuzi hayo kikilenga kujadili mbinu za kulinda uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi.
Waziri wa Habari na Mawasiliano, Cornelius Mweetwa, amesema hatua hizo ni za muda mfupi zenye lengo la kupunguza athari zinazotokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

Amesema, "hali ya mvutano inayoendelea Mashariki ya Kati imechangia kupungua kwa upatikanaji wa mafuta, hali iliyosababisha bei kupanda kimataifa na ndani ya Zambia."
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuwafahamisha wananchi kuhusu juhudi zinazochukuliwa, ili kulinda maisha yao, biashara, na sekta nyeti dhidi ya gharama kubwa za mafuta.
"Baraza la Mawaziri limeidhinisha kuondolewa kwa VAT na kusimamishwa kwa ushuru huo kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia usiku wa Jumatatu," alisisitiza Mweetwa.
Hata hivyo alibainisha kuwa, bila hatua hizo kuchukuliwa bei za mafuta kwa mwezi Aprili zingepanda kwa kiwango kikubwa na hivyo kuongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions