Na Adam Msafiri - Mara.
Wakazi wa Wilaya ya Butiama mkoani Mara wameibua kilio cha ukosefu wa huduma ya umeme katika zaidi ya vitongoji 100, wakisema changamoto hiyo imekuwa ikikwamisha shughuli za maendeleo na maisha yao ya kila siku.
Malalamiko hayo yametolewa mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati akiendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Mara, ambapo wananchi walisema licha ya ahadi mbalimbali za Serikali, bado vitongoji vingi havijafikiwa na huduma hiyo muhimu.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mwenge wilayani Butiama, baadhi ya wananchi akiwemo Deus Esore na Juma Mirumbe, wameomba Serikali kuharakisha usambazaji wa umeme katika vitongoji vilivyosalia, wakieleza kuwa ukosefu wa nishati hiyo unarudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo, akieleza kuwa vijiji vyote vya Wilaya ya Butiama tayari vimeunganishwa na umeme, huku baadhi ya vitongoji pekee vikisalia bila huduma hiyo. Alisema Serikali inaendelea na mipango ya kuhakikisha vitongoji hivyo navyo vinafikiwa.

Akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kutekeleza miradi ya usambazaji wa umeme nchini, akiahidi kuwa hakuna kijiji wala kitongoji kitakachoachwa nyuma katika juhudi za kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya umeme.

Mbali na suala la umeme, Dkt. Nchemba aliwataka Watanzania kuendelea kulinda na kudumisha amani na utulivu wa nchi, akisema ndiyo msingi muhimu wa maendeleo ya taifa.
Discussion
Reader comments
0 contributions