Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma imenufaika na mradi wa nishati safi ya kupikia wenye thamani ya shilingi milioni 212.4, unaofadhiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani (WFP), kwa lengo la kuimarisha matumizi ya nishati safi katika shule za msingi, kupunguza matumizi ya kuni na kulinda mazingira.
Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo, shule tatu za msingi zimepatiwa huduma za nishati safi ya kupikia ambazo ni Shule ya Msingi Murubona iliyopatiwa Shilingi milioni 72.6, Shule ya Msingi Mwibuye Shilingi milioni 72.6 na Shule ya Msingi Kabanga Mazoezi iliyopatiwa Shilingi milioni 67.2.

Mradi huo ulianza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 na kwa sasa umekabidhiwa rasmi kwa wahusika. Utekelezaji wake umejumuisha utoaji wa mafunzo kwa walimu na wapishi, ukarabati wa majengo ya majiko pamoja na ununuzi na ufungaji wa majiko ya kisasa ya teknolojia ya Pressure Cooker.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Afisa Utumishi, Daniel Kaloza, ameishukuru WFP kwa kufadhili mradi huo ambao unaunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira.

Aidha, ameomba ushirikiano kati ya Halmashauri na WFP uendelee kuimarishwa ili kutoa fursa kwa shule nyingine kunufaika na miradi ya aina hiyo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi (Energy Advisor) kutoka WFP, Geoffrey Ndegwa, ameishukuru Halmashauri ya Mji Kasulu kwa ushirikiano mzuri uliowezesha utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo kadiri fursa nyingine zitakapopatikana.

Mradi huo unatarajiwa kuchangia kuboresha mazingira ya upishi shuleni, kupunguza gharama na matumizi ya kuni, kuimarisha afya ya wapishi na wanafunzi pamoja na kuunga mkono juhudi za kitaifa za matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Discussion
Reader comments
0 contributions