Na Saada Almasi – Simiyu.
Zaidi ya majangili 20 wamekamatwa katika kipindi cha Januari hadi Mei mwaka huu ambao wamekuwa wakiingia kinyemela katika hifadhi ya wanyama Serengeti mkoani Simiyu na kufanya shughuli za uwindaji bila kufuata sheria.
Akitoa ripoti hiyo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Afisa Mhifadhi Daraja la Kwanza Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, David Sule amesema kuwa majangili hao wamekuwa wakiingia hifadhini kupitia lango kuu la kijiji cha Damidami, Halawa Gibishi na kijiji cha Chungu vijiji ambavyo vipo karibu na hifadhi hiyo kabla ya kuingia hifadhini na kufanya uharibifu huo.
“Vijiji vya jirani na hapa ndivyo hasa vimekuwa lango la hawa majangili ambao hadi sasa 22 tumewatia baroni japokuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya wanankjiji kuendelea kufumbia macho taarifa za hawa watu punde tu wanapofika katika maeneo yao,hivyo niwaombe wanakijiji tushirikiane katika hili,” amesema David.
Kufuatia suala hili mkuu wa wilaya ya Bariadi Simon Simalenga ametoa onyo kwa wakazi hao kuhakikisha wanatoa taarifa za wavamizi hao wasio na nia nzuri na wanyama kwani kutofanya hivyo kutasababisha hatua kali kuchukuliwa dhidi yao.

“Unajisikiaje unapoona mnyama kama tembo katolewa mkonga wake kakatwa mkia ametelekezwa hifadhini na wewe unamjua aliyefanya hivyo lakini upo kimya sasa nitoe onyo yeyote ambaye atabainika kufumbia macho taarifa za wavamizi tutamchukulia hatua za kisheria yeye na huyo mtu anayemficha, nawasihi hili lisijirudie tena,” amesema DC Simalenga.
Hata hivyo, wananchi hao wametoa kilio chao cha muda mrefu cha uvamizi wa wanyama tembo katika makazi na mashamba yao hali ambayo inawarudisha nyuma kimaendeleo ndipo Simalenga akawatia moyo kwa kuwapa mikakati ya serikali ya kudhibiti wanyama hao.

“Mpango wa serikali uliopo ni kupiga fensi ya umeme katika maeneo yote ya pori la akiba Maswa,Kijereshi na hifadhi ya Serengeti kwa hivyo ni suala la muda tu wanyama wote watabaki katika maeneo yao ya mipaka na wananchi pia mtabaki katika maeneo yenu kwa hiyo tambueni serikali ipo na inajua kilio chenu,” ameongeza DC Simalenga.
Discussion
Reader comments
0 contributions