Zaidi ya kaya elfu ishirini na sita zinatarajiwa kusajiliwa na kupatiwa kadi za bima ya afya kwa wote kupitia usajili wa awamu ya pili ambao umezinduliwa hii leo October 22,2026 Mkoani Kigoma.
Baadhi ya wanannchi wa Kata ya Rusimbi Manispaa ya Kigoma Ujiji wakizungumza na Jambo Fm, wakati wa zoezi la uzinduzi la usajili wa kaya wamesema bima hizo zitawasaidia kupata huduma za afya kwa uhakika kwani hapo awali walikuwa wakitumia gharama kubwa za matibabu na wakati mwingine kushindwa kabisa kumudu.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro akisalimiana na baadhi wananchi walijitokeza katika uzinduzi wa bima ya afya kwa wote
Rashid Masoud na Rehema Rephael ni miongoni mwa wananchi watakaonufaika na bima ya afya kwa wote wamesema awali walikuwa wakihangaika kupata matibabu kutokana na kipato cha familia zao kuwa masikini.
Naye Meneja wa NHIF Mkoa wa Kigoma Gwamaka Mwakyoma amesema katika awamu hii ya pili uzinduzi wa bima ya afya watahakikisha wanafikia lengo walilojiwekea la kufikia kaya zaidi ya elfu 22 kwa ajili ya usajili wa bima ya afya kwa wote.

Meneja wa NHIF Mkoa wa Kigoma Gwamaka Mwakyoma, Picha na Tryphone Odace
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya bima ya afya kwa wote, Mkuu wa mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro aliwataka wananchi kuchangia kiasi cha shilingi 150,000 kwa kila kaya yenye idadi ya watu hadi sita ili waweze kukidhi kigezo cha kupatiwa huduma kupitia bima ya afya kwa wote.
Balozi Sirro alisema ni muhimu wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kujiunga na bima ya afya kwa wote ili kuwa na uhakika wa kupata matibabuwanapokuwa na changamoto za ugonjwa.

Mkuu wa Mkoa Kigoma akifurahia jambo na mmoja wa wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa bima ya afya, Picha na Tryphone Odace
Aidha Mkuu wa Mkoa Sirro alitoa maelekezo kwa watendaji wa halmashauri zote kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki za afya pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi watakaobainika kukiuka utaratibu uliowekwa.
Uzinduzi wa usajili wa Bima ya afya kwa wote awamu ya pili kwa mkoa wa Kigoma umefanyika hii leo katika Manispaa ya Kigoma ujiji huku kitaifa ukifanyika mkoani Mtwara.
Discussion
Reader comments
0 contributions