Na Saada Almasi, Bariadi - Simiyu.
Zaidi ya wakazi 12,000 waishio katika Kijiji cha Mwabadimu Kata ya Nkololo Wilayani Bariadi mkoani Simiyu, wanakwenda kunufaika na uwepo wa Zahanati ya Mwabadimu ambayo imejengwa na serikali kwa gharama ya shilingi milioni 270 ikiwa ni pamoja na nyumba mbili za watumishi.
Awali, wakazi wa Kata hiyo walilazimika kutembea umbali wa kilometa 3 hadi 10 kufuata huduma za afya katika maeneo mengine hali ambayo iliwalazimu kutoa gharama kubwa za usafiri na hata kupoteza maisha pale ambapo mtu ameugua usiku na kutakiwa kupatiwa huduma za haraka.

Akizindua Zahanati hiyo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2026 Wazo Mwang’onda baada ya kukagua Miundombinu ya Zahanati hiyo amesema, ameridhishwa na ujenzi uliofanyika.
“Tumeona jengo letu la zahanati linapendeza na limejengwa kwa ubora wa hali ya juu na kwa kuliangalia kwa haraka unaweza kuhisi ni kituo cha afya ,niwapongeze sana hii inaonyesha kwa vitendo dhamira ya serikali kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora za afya na utekelezaji huu utaendelea kila kata kila kijiji ili wananchi mpate huduma karibu nisisitize tu muendelee kulinda amani ya nchi,” amesema Mwang’onda.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Pelila Zambi amesema kuwa wananchi wa maeneo hayo walilazimika kutembea umbali mrefu kifuata huduma za afya lakini kwa sasa wanakwenda kuwa na uhakika wa afya zao.
“Nikiri kuwa changamoto ya huduma za afya eneo hili ilikuwa ni kubwa maana wananchi wasio na uwezo kifedha walilazimika kutembea kwa miguu kufuata huduma maeneo ambayo ni mbali na hapa,sasa tayari unaumwa na unatembea kufuata tiba ule mwendo tu unaongeza ugonjwa labda mtu uwe na pesa za usafiri tofauti na hapo lolote linaweza kutokea,lakini kwa uwepo wa zahanati hii unakwenda kuokoa maisha ya wengi,” amesema Zambi
Discussion
Reader comments
0 contributions