Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM) Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, wameanza zoezi la usajili wa watu wenye ulemavu kwenye mfumo wa kidijitali (PDMIS) mkoani humo.
Zoezi hilo linalenga kufikia zaidi ya watu 5,000, likianza katika Manispaa ya Shinyanga kwa kuwajengea uwezo Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa TEHAMA ngazi ya Halmashauri na Kata ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa wa ufanisi.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Mwandamizi kutoka OWM, Joy Maongezi, amesema hatua hiyo inalenga kuwatambua rasmi watu wenye ulemavu na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za maendeleo, ikiwemo mikopo na huduma za kijamii.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga, Lydia Kwesigabo, amesema zoezi hilo litaanza kwa siku mbili katika kata mbili za Manispaa ya Shinyanga na baadaye kuendelea katika maeneo yote ya mkoa.

Aidha, Afisa TEHAMA kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Dickson Chibululu ameeleza kuwa matumizi ya mfumo huo wa kidijitali yataongeza upatikanaji wa takwimu sahihi na kupunguza gharama za uendeshaji wa huduma za serikali.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Mkoa wa Shinyanga, Mzee Richard Mpongo, amepongeza hatua hiyo akieleza kuwa itasaidia kuongeza utambuzi na upatikanaji wa fursa kwa kundi hilo muhimu.

Discussion
Reader comments
0 contributions