Na Daniel Gahu – Katavi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limewataka wananchi wenye silaha haramu au silaha zinazotumika kinyume na taratibu za kisheria kuzisalimisha kwa hiari, katika kampeni maalum inayolenga kuimarisha amani na usalama katika mkoa huo.
Kampeni hiyo imeanza rasmi Septemba 1, 2026 na inatarajiwa kuendelea hadi Oktoba 31, 2026, kufuatia uzinduzi wa zoezi la usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari uliofanywa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Paschal Patrobas Katambi, Agosti 31, 2026.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, kampeni hiyo inalenga kuwahamasisha wananchi wenye silaha zinazomilikiwa bila uhalali wa kisheria, silaha za watu waliofariki ambazo hazijasalimishwa, pamoja na silaha za watu waliopoteza sifa za kuzimiliki kutokana na sababu za kiafya au umri, kuzisalimisha kwa hiari.
Aidha, silaha zinazolengwa katika zoezi hilo ni pamoja na zile zinazomilikiwa kihalali lakini zikitumika katika matukio ya kihalifu, pamoja na silaha zilizotengenezwa kienyeji na kutumika kinyume na sheria.
Jeshi hilo limewataka wananchi kutumia fursa hiyo kuzisalimisha silaha hizo katika vituo vya Polisi, Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Ofisi za Wenyeviti wa Serikali za Mitaa au sehemu nyingine za wazi zitakazotangazwa na mamlaka husika na ambazo zinapatikana kwa urahisi.
Jeshi la Polisi limeonya kuwa baada ya kukamilika kwa kipindi cha usalimishaji wa hiari, operesheni maalum itafanyika kuwasaka na kuwakamata watu watakaokuwa wamekaidi fursa hiyo, ambapo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa kuhusu uwepo wa silaha haramu au watu wanaozimiliki, ili kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa na kuzuia matumizi ya silaha hizo katika uhalifu.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa, huku likisisitiza kuwa lengo kuu ni kupunguza uwepo wa silaha haramu mikononi mwa watu na hatimaye kuimarisha amani, usalama na utulivu mkoani Katavi.

Discussion
Reader comments
0 contributions