Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka wazee nchini kutumia hekima na uzoefu wao katika kuimarisha malezi, maadili na mshikamano wa familia, akisisitiza kuwa nafasi yao katika jamii si ya ushauri pekee bali ni sehemu muhimu ya kujenga kizazi chenye maadili.
Dkt. Gwajima amesema hayo Oktoba 02,2026 jijini Dodoma kwenye kikao cha mabaraza ya ushauri ya wazee ngazi ya taifa na kueleza kuwa wazee wana nafasi ya kipekee katika kujenga familia imara, jamii imara na Taifa imara.
"Mabaraza ya Wazee yanapaswa kwenda zaidi ya kuwa majukwaa ya kukutana na kujadili changamoto pamoja na kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii,"amesema.

Kwa mujibu wa Waziri Gwajima, wazee wanapaswa kushirikiana na familia, jamii, shule, viongozi wa dini na Serikali za Mitaa katika kuwaongoza vijana kuhusu maadili, uzalendo, mila na desturi njema, ili tunu hizo ziweze kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
"Nizitake familia zetu kurejesha nafasi ya wazee katika malezi na ushauri, huku wazee mkitumia nafasi hiyo kuwa nguzo ya maridhiano, mshikamano na utatuzi wa changamoto ndani ya familia,"amesema.
Dkt. Gwajima pia ametoa maelekezo ya kuhuishwa na kuimarishwa kwa Mabaraza ya Wazee katika ngazi zote, pamoja na kuanzishwa na kuimarishwa kwa klabu za mazoezi kwa wazee ili kuwawezesha kujenga afya na kupata elimu kuhusu afya, lishe, haki na ustawi wao.

Awali akisoma maazimio ya Baraza, Mjumbe wa baraza hilo Mzee Livingstone Byekwaso amesema wameazimia kuishauri Serikali kuanzisha pensheni ya jamii kwa wazee wenye umri wa miaka 70 na kuendelea, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa kipato na ustawi wa wazee nchini.
Azimio hilo ni miongoni mwa maazimio 17 yaliyofikiwa katika kikao cha Baraza la Wazee Taifa, huku likitaka utekelezaji wa mpango huo uzingatie uzoefu wa Zanzibar katika utoaji wa pensheni ya jamii kwa wazee.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la ushauri la Wazee Mzee David Sendo amesema wataendelea kushirikiana n Wizara ili kuhakikisha yale yote waliyojadili kupitia kikao cha siku mbili yanatekelezeka.
Discussion
Reader comments
0 contributions