Skip to main content

WAZAZI WATAKIWA KUWAFUNDISHA WATOTO STADI YA KAZI ILI KUZIKABILI CHANGAMOTO ZA AJIRA

Na Daniel Gahu - Katavi.

WAZAZI WATAKIWA KUWAFUNDISHA WATOTO STADI YA KAZI ILI KUZIKABILI CHANGAMOTO ZA AJIRA

Na Daniel Gahu - Katavi.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdalla Hamid, amewataka watendaji wote wa Serikali nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na kujituma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kupunguza malalamiko yanayojitokeza katika utoaji wa huduma za umma.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na makundi mbalimbali ya wananchi mkoani Katavi, Rabia amesema kuwa Serikali imeweka mazingira mazuri ya kuwahudumia wananchi, hivyo ni wajibu wa watendaji kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa wakati, kwa haki na kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Amesisitiza kuwa utendaji wenye uwajibikaji utasaidia kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali pamoja na kuongeza kasi ya maendeleo katika sekta mbalimbali.

Mbali na hilo, Rabia ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwajengea watoto wao utamaduni wa kujifunza stadi za kazi za mikono tangu wakiwa wadogo. Amesema ujuzi katika fani mbalimbali kama ususi, unyoaji, ushonaji, ufundi pamoja na kazi nyingine za ujasiriamali ni nyenzo muhimu zitakazowawezesha vijana kujiajiri na kupunguza utegemezi wa ajira rasmi.

Ameeleza kuwa pamoja na elimu ya darasani, ujuzi wa vitendo ni msingi muhimu wa kujenga uchumi wa mtu binafsi na Taifa kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa vijana wanapaswa kuandaliwa kuwa wabunifu na wazalishaji wa fursa za ajira badala ya kusubiri kuajiriwa.

Katika hatua nyingine, Katibu huyo wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi (RMO) kuhakikisha wananchi wa mkoa huo wanapata huduma bora za afya, zenye ubora, zinazopatikana kwa wakati na zinazokidhi mahitaji ya wananchi wote bila ubaguzi.

Amesema sekta ya afya ni moja ya maeneo muhimu yanayogusa maisha ya kila siku ya wananchi, hivyo viongozi na watendaji wa sekta hiyo wanapaswa kuhakikisha huduma zinaboreshwa na changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Wakati wa ziara hiyo, Rabia alipata nafasi ya kusikiliza maoni, changamoto na kero mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi kutoka makundi tofauti ya kijamii.

Miongoni mwa kero zilizoibuliwa ni malalamiko kuhusu kile walichodai kuwa ni ukaguzi holela unaofanywa na baadhi ya maafisa wa Serikali katika migahawa ya Mama Lishe na Baba Lishe, huku ukaguzi huo ukiambatana na askari wa Jeshi la Polisi, jambo ambalo wafanyabiashara hao walisema linawatia hofu na kuathiri shughuli zao za kila siku.

Baada ya kupokea malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Hozza Mrindoko amekemea tabia hiyo na kutoa maelekezo ya kupiga marufuku maafisa wa Serikali kufanya ukaguzi wa kawaida wakiwa wameambatana na askari polisi, isipokuwa pale ambapo mazingira ya kiusalama yanahitaji kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria na taratibu husika.

Makundi yaliyoshiriki kutoa maoni na kero katika mkutano huo ni pamoja na viongozi wa dini, wazee, Sungusungu, machifu, wakulima, wafugaji, wachimbaji wa madini, mafundi gereji, mafundi ujenzi, wanamichezo, wavuvi, wanafunzi wa vyuo, walimu, machinga, mawinga, wafanyabiashara, Mama Lishe, Baba Lishe, vyama vya ushirika, maafisa usafirishaji pamoja na vikundi mbalimbali vya ujasiriamali.

Ziara hiyo imekuwa sehemu ya juhudi za viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kusikiliza kero za wananchi, kufuatilia utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kutoa maelekezo yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma za Serikali pamoja na kuimarisha ustawi wa wananchi.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.