Na Gideon Gregory - Dodoma.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema moja ya suala linaloumiza ni kitendo cha uwepo wa taasisi za wazawa zinazoweza kutekeleza miradi na pengine zenye uwezo mkubwa kuliko za kigeni, lakini linapokuja suala la kupewa zabuni zinakwenda kwa wageni.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo Aprili 8, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025.
Ameongeza kuwa yapo mataifa ambayo hayajawahi kuipa Tanzania hata msaada wa mkopo kwa kipindi cha hadi miaka 10, halafu zaidi ya shilingi trilioni 70 za mapato zinakwenda kwenye miradi ya kampuni za nchi hizo baada ya kupewa zabuni!

“Maana yake nini, nyie mnakuwa mnahangaika kukusanya fedha kupitia maduhuli, huku mamlaka ya mapato mnakusanya, halafu mnakwenda kuwarundikia wale wapeleke kwenye nchi yao. Wanakuza huko nchini kwao,” amesema.
Pia amesisitiza kuwa uwepo wa sera, sheria na kanuni bora hauwezi kuleta matokeo chanya iwapo utekelezaji wake hautakuwa makini na wenye uwajibikaji, akionya dhidi ya tabia ya kuwa na nyaraka nzuri zisizotekelezwa ipasavyo.
“Sasa tunapoleta sera hii tusitwange maji kwenye kinu, tusiwe na kitu kizuri kimeandikwa, sera nzuri imeandikwa, sheria nzuri imeandikwa, kanuni nzuri zimeandikwa, halafu tukienda kwenye uhalisia mambo yawe kama kawaida,” amesisitiza.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameeleza kuwa vitendo vya rushwa katika usimamizi wa mnyororo wa ugavi katika sekta ya umma vinaendelea kuwa changamoto kubwa, sambamba na matatizo mengine ya kiutendaji yanayohitaji kushughulikiwa kwa umakini ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji.
“Zikisimamiwa vyema, fedha chache tulizonazo zinaweza kutufikisha mbali zaidi katika kuwahudumia wananchi na kuimarisha maendeleo ya taifa letu,” amesema.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha usimamizi wa rasilimali na kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta matokeo chanya kwa wananchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions