Jeshi la Polisi mkoani Iringa, linawashikilia watuhumiwa wawili wa mtandao wa utapeli, uliokuwa ukitumia majina ya kampuni za Alliance in Motion Global na QNET, kuwarubuni vijana 75 kwa ahadi ya kuwapatia ajira.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP. Allan Bukumbi amewataja watuhumiwa hao kuwani Jackson Kalu (26) mjasiliamali mkazi wa Bahi Dodoma na Michael Mfuse (32) mkazi wa Wanging’ombe Njombe, wakitumia gari aina ya BMW X1 kwa kazi hiyo haramu.

Amesema,Wahanga hao, ambao wengi wao ni vijana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 30, wanatoka mikoa ya Dodoma, Mwanza, Lindi, Njombe, Mtwara pamoja na Mafia.
Kamanda Bukumbi amesema kuwa vijana hao 75 walikuwa wakichangishwa fedha zaidi shilingi laki sita mpaka milioni nne, kama kiingilio kinyume na sheria.

"Uchunguzi umebaini kuwa vijana hao wamekuwa wakiishi katika mazingira yasiyofaa, ambapo zaidi ya watu 10 hulazimika kulala katika chumba kimoja wakati wakisubiri kuanza shughuli hizo haramu, jambo linalokiuka sheria na kanuni za nchi," alisema Kamanda Bukumbi.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda Bukumbi amewataka wazazi na walezi kufuatilia watoto wao kwa karibu na kufika Kituo Kikuu cha Polisi Iringa kuwatambua huku baadhi ya vijana waliorubuniwa wakisema waliambiwa wakijiunga na mtandao huo watapata faida.
Discussion
Reader comments
0 contributions