Watu wawili wamefariki dunia na magari mawili kuharibika baada ya gari aina ya Toyota Harrier kugongana na pikipiki katika barabara ya Singida–Veta, mjini Singida.
Taarifa iliyotolewa Novemba 2, 2026, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Matride Kuyeto imeeleza kuwa ajali hiyo imetokea Novemba 1, 2026, majira ya saa 5:10 usiku katika eneo la Veta, Kata ya Utemini, Manispaa ya Singida.
Gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 757 EBJ, lililokuwa likiendeshwa na Athumani Mkalimoto (42), mfanyakazi wa SUWASA na mkazi wa Mwaja, liligongana na pikipiki yenye namba MC 131 FNY aina ya Haojue, iliyokuwa ikiendeshwa na Selemani Athumani Hamis (27), mkazi wa Veta.
Kamanda Kuyeto amewataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Selemani Athumani Hamis (27), dereva wa pikipiki hiyo, pamoja na Athumani Hamis (53), Diwani wa Kata ya Kinyangiri, Wilaya ya Mkalama, aliyekuwa abiria kwenye pikipiki hiyo. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Manispaa ya Singida.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Matride Kuyeto
Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Toyota Harrier, ambaye alijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari za usalama, na hivyo kugonga pikipiki hiyo na kusababisha vifo na uharibifu wa vyombo hivyo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linaendelea kutoa wito kwa madereva na watumiaji wa vyombo vya moto vya moto vya moto vya barabarani kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, ikiwemo kuepuka mwendo kasi na kufanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha yao na watumiaji wengine wa barabara.
Discussion
Reader comments
0 contributions