Na Ibrahim Rojala - Geita.
Watu wawili wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa kufuatia ajali iliyohusisha magari mawili iliyotokea Mei 17,2026 katika Kijiji cha Msasa, Kata ya Runzewe Magharibi, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi Mkoa wa Geita Mei 18, 2026 imeelezwa kuwa ajali hiyo ilitokea Mei 17,2026 majira ya saa 12:00 jioni ikihusisha gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T631 DSE ambalo liligonga kwa nyuma lori aina ya Scania lenye namba za usajili T484 CTX, lililokuwa likiendeshwa na Natale Joseph (55), mkazi wa Dodoma.
Taarifa hiyo imewataja waliopoteza maisha kuwa ni, Silas Edward (48), aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota Harrier, pamoja na abiria Peluzi Ndakama (29), wote wakazi wa Katoro,majeruhi akiiwa ni Feruzi Shome (25) aliyepata majeraha na anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.

Chanzo cha ajali hiyo kimeelezwa kuwa ni dereva wa gari Toyota Harrier (T631 DSE) kuendesha kwa mwendo kasi bila kuzingatia tahadhari za usalama barabarani, hali iliyosababisha kushindwa kulimudu gari hilo na kuligonga kwa nyuma lori aina ya Scania lililokuwa mbele yake.
Jeshi la Polisi mkoani Geita limetoa rai kwa madereva na watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuepuka mwendo kasi, pamoja na kufuata alama na maelekezo ya usalama ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.
Discussion
Reader comments
0 contributions