Serikali imeshauriwa kuwekeza katika teknolojia ya kuhifadhi samaki, hususan uzalishaji wa barafu kwa kutumia nishati ya jua ili kupunguza gharama za uhifadhi wa mazao ya uvuvi na kuongeza kipato cha wavuvi na wafanyabiashara wa samaki Mkoani Kigoma.
Mratibu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi, Hashim Muumin, alisema kuwa licha ya barafu kuwa na umuhimu mkubwa katika kuhifadhi samaki baada ya kuvuliwa, gharama kubwa za umeme zimekuwa kikwazo kwa baadhi ya wavuvi na wafanyabiashara kutumia teknolojia hiyo.

Muonekano wa vifaa vya kuhifadhi samaki wakiwa wamevulia
Alisema hali hiyo inachangia upotevu wa samaki, jambo linaloweza kupunguza mapato ya wadau wa sekta ya uvuvi.
Kwa upande wao, baadhi ya wafanyabiashara na wadau wa uvuvi walisema matumizi ya nishati ya jua katika uzalishaji wa barafu yanaweza kupunguza gharama za uendeshaji na kuboresha uhifadhi wa samaki, hatua itakayowanufaisha wavuvi, wafanyabiashara pamoja na walaji.
Walisema teknolojia hiyo ikitumika ipasavyo itasaidia kupunguza upotevu wa samaki na kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi, hivyo kuwawezesha wadau kupata faida zaidi.

Muonekano wa samaki wakiwa tayari wamefikishwa soko mjini Kigoma
Naye Afisa Uvuvi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Edmound Kajuni, alisema Serikali tayari imetenga bajeti kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa nishati ya kuhifadhi mazao ya uvuvi kwa wafanyabiashara na wavuvi.
Alisema hatua hiyo inalenga kuboresha mazingira ya uhifadhi wa samaki na kusaidia wadau wa sekta hiyo kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Muonekano wa vifaa vya kuhifadhi samaki ambavyo vinatajwa kuwa havikidhi ubora
Kwa ujumla, uwekezaji katika teknolojia ya uzalishaji wa barafu kwa kutumia nishati ya jua unatajwa kuwa miongoni mwa hatua zinazoweza kusaidia kupunguza gharama za uhifadhi, kupunguza upotevu wa samaki na kuongeza kipato kwa wadau wa sekta ya uvuvi mkoani Kigoma.
Discussion
Reader comments
0 contributions