Watumishi wapya 402 wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, wamekumbushwa kuzingatia wajibu na maadili ya Utumishi wa Umma, ili kuhakikisha wanatoa huduma bora, zenye ufanisi na zinazokidhi mahitaji ya wananchi.
Akizungumza wakati wa mafunzo maalumu kwa watumishi hao yaliyofanyika mjini Igunga, Mkufunzi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Singida, Emmanuel Masewa, amesema watumishi wa umma wanapaswa kuzingatia sheria za nchi, sheria za Utumishi wa Umma pamoja na kanuni na maadili yanayoongoza utendaji wao.
Masewa amesisitiza kuwa watumishi hao wana wajibu wa kuwahudumia wananchi na wateja wengine kwa uaminifu, uadilifu, ukarimu na upole, huku akiwataka kuhakikisha wanachangia kuboresha huduma zinazotolewa na waajiri wao. Aidha, amewakumbusha kutunza siri za ofisi na za nchi, kuheshimu maadili ya taaluma zao na kutumia rasilimali za umma kwa uangalifu na uwajibikaji.
Ameongeza kuwa kuzingatia nidhamu, kuheshimu mamlaka za ajira na kufuata taratibu za kiutumishi ni miongoni mwa misingi muhimu inayopaswa kuzingatiwa na kila mtumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yake.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Zaituni Kisusi, amewahakikishia watumishi hao kuwa ofisi yake itaendelea kuwahudumia na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Katika mafunzo hayo, watumishi hao wamepatiwa elimu kuhusu muundo wa Serikali na majukumu yake, maadili ya utendaji katika Utumishi wa Umma, Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2018 pamoja na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, ikiwa ni sehemu ya kuwaandaa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, taratibu na misingi ya utumishi bora.
Discussion
Reader comments
0 contributions