Na William Bundala, Kahama - Shinyanga.
Watumishi wa manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga wametakiwa kuwa na umoja na mshikamano ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku kwa lengo la kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Ndg Masudi Kibetu wakati akizungumza na watumishi wa manispaa ya Kahama katika ukumbi wa mikutano wa manispaa hiyo.

Kibetu amesema Mshikamano na umoja ndiyo nguzo kubwa ya kuleta ufanisi katika kazi na kuwataka watumishi hao kuwa wamoja na kuzingatia sheria kanuni na maadili ya utumishi wa umma.
“Tupo Idara tofauti katika manispaa yetu,lakini tukishirikiana kwa Pamoja na kuwa na lengo moja nina hakika tutakuwa na ufanisi mkubwa wa utendaji kazi katika manispaa yetu huku tukizingatia taratibu zote za maadili ya utumishi wa Umma” Amesema Kibetu.

Kibetu ameongeza kuwa bila kuwa na mshikamano na umoja ni vigumu kufikia malengo waliyojiwekea kwani tasisi za umma zinategemena katika kufikia dhima ya jambo fulani katika kuleta maendeleo.
“Taasisi zetu zinategemeana na ili kufikia malengo ni lazima tuwe na umoja na mshikamo Pamoja na upendo kati yetu,hii itatufanya tujue wajibu wetu na wakati mwingine tukumbushane majukumu na wajbu katika Idara zetu” Ameongeza Kibetu.

Katika hatua nyingine Kibetu amewataka Watumishi wa Manispaa ya Kahama kujiandaa kwa Mapokezi ya Mwenge wa Uhuru utakaoingia Mwezi Agosti na kusisitiza kuweka Uzalendo mbele.
“Kama mnavyojua mwenge wa Uhuru unatarajia kuwa wilayani kwetu Mwezi Agosti,niwaombe kila mtumishi ajiandae kwa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru na niwaombe sana tuwe wazalendo na tushiriki kila mmoja kwa nafasi yake ili kuhakikisha mwaka huu tunapata ushindi mkubwa wa mapokezi ya Mwenge wa uhuru kimkoa hata kitaifa” Amesisitiza Kibetu.

Nao baadhi ya watumishi wa manispaa ya Kahama waliohudhuria kikao hicho wamesema wamepokea kwa utekelezaji maagizo yote yalitolewa na mkurugenzi na kwamba watayafanyia kazi huku wakimpongeza kwa kuwakumbusha mara kwa mara wajibu na taratibu za utumishi wa umma.

“Tumeyapokea yote yaliyotolewa na mkurugenzi wetu na tunahaidi kuyafanyia kazi kwa nafasi zetu,lakini tunamshukuru sana amekuwa mstari wa mbele kutukumbusha mara kwa mara wajibu na utaratibu wa utumishi wa umma na tuna hakika sote tukiwa na dhamira moja na mshikamo tutakuwa na ufanisi mkubwa” Wamesema watumishi hao.

Discussion
Reader comments
0 contributions