Na Daniel Gahu - Katavi.
Burudani, Shangwe, ushindani wa kirafiki na ari ya kujenga afya vimetawala katika bonanza la michezo lililoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kukutanisha watumishi kutoka mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora, likiwa jukwaa la kuimarisha mshikamano, ushirikiano na kubadilishana uzoefu miongoni mwa watumishi wa kanda ya Nyanda za Magharibi.
Akifungua bonanza hilo lililofanyika mkoani Katavi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Albert Msovela, amesema kuwa michezo ni sehemu muhimu ya maisha ya mtumishi kwani huimarisha afya ya mwili na akili, huondoa msongo wa mawazo pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

“Tunapaswa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara kwa sababu afya njema ndiyo msingi wa utendaji kazi wenye tija. Bonanza hili limetupa fursa ya kuimarisha ushirikiano, kujifunza kutoka kwa wenzetu na kujenga mshikamano utakaotusaidia kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi,” amesema Bw. Msovela.
Aidha amesema, katika kipindi hiki ambacho watumishi wengi hutumia muda mwingi wakiwa ofisini, ni muhimu kuendelea kuhamasisha ushiriki wa michezo na mazoezi ili kujikinga dhidi ya changamoto za kiafya zinazotokana na mtindo wa maisha usiozingatia mazoezi.

Ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kuandaa bonanza hilo, akieleza kuwa michezo si tu huimarisha afya za watumishi bali pia hujenga umoja, nidhamu, ushirikiano na kuongeza ari ya kazi inayochangia utoaji bora wa huduma kwa wananchi.
Bonanza hilo limehusisha michezo mbalimbali na kuendelea kudhihirisha nafasi ya michezo kama nyenzo muhimu ya kuunganisha watumishi, kuimarisha ustawi wao na kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu ya umma.






Discussion
Reader comments
0 contributions