Na Saada Almasi, Itilima - Simiyu.
Watumishi wapya 120 wa kada mbalimbali Wilayani Itilima Mkoani Simiyu, ambao wameingia katika ajira Novemba 25 na Machi 2026 bila kupata mafunzo elekezi wamepewa mafunzo jumuishi ya utumishi, ili kuendana na Dira na Misingi ya Kiutumishi katika Halmashauri zilizo chini ya Serikali za Mitaa.
Akifungua mafunzo hayo ya siku moja, yaliyofanyika wilayani humo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri hiyo, Mateso Paul amesema kupitia maelekezo watakayopata watayatumia kama chachu ya kuendana na mabadiliko ya mazingira, ili kufikisha huduma bora kwa Wananchi.
“Tunatambua kuwa mmetoka vyuoni maeneo mbalimbali huku mmekutana na mazingira mapya ili muweze kufanikiwa mnatakiwa kuendana na mazingira mnayoyakuta,wananchi wanatarajia huduma bora kutoka kwenu bila kujitambua nyie wenyewe hamuwezi kufikisha kusudio la Serikali kwa wananchi wake,” amesema Mateso.

Ameongeza kuwa, ”kwa kuwatazama sura zenu mnapendeza ,sitarajii tukutane hapa baada ya mwaka mmoja nibaini majanga ya kupigwa kwa wizi,fumanizi,na hata ulevi ni aibu utapoteza kibarua chako kwa mambo ya kijinga nataka mjipange,muandae kesho yenu kwa kujiwekeza katika mipango mizuri.”
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala Wilayani humo, Polycarp Ntapanya amesema kuwa katika kila Halmashauri ambayo ipo chini ya mfumo wa Serikali za Mitaa (LGAs) ina utaratibu wake ambao kila mtumishi anapaswa kuufuata hiyo kuwaweka pamoja kunaondoa mianya ya utofauti ndani yao.
“Halmashauri zina utaratibu wake na mamlaka kamili hivyo tunapowapokea lazima tuwaelekeze kufuata mila na taratibu ambazo zinatumika kuhudumia wananchi pia wajue ni idara zipi wanazitumikia hivyo tunavunja vunja tofauti zao walizotoka nazo vyuoni na wawe wamoja pia tunawaelekeza kuhusiana na kesho yao kwani kila anayeingia kazini anapaswa kujiandaa kustaafu,” amesema Polycarp.

Naye Mwakilishi kutoka mfuko wa hifadhi ya jamii PSSSF amesema kuwa katika kila nafasi aliyonayo mtumishi ni lazima atambue kuwa zipo taasisi ambazo zinamsimamia kuhakikisha amestaafu na kulipwa stahiki zake ambazo ni michango yake anayoitoka pindi anapokuwa katika ajira
“Wanaisikia hii mifuko lakini namna gani inafanya kazi hawajui sasa uwepo wetu hapa unawafumbua macho kuona namna nzuri ya kujiunga na namna ya kuchangia kwa faida yao wenyewe na familia zao,” amesema Charles Muhoni Afisa matekelezo PSSSF.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamezungumza na Jambo Fm na kusema wamepata faida kubwa baada ya mafunzo hayo, kwani wengi wao hawakujua namna bora ya kuendana na mazingira ya kazi zao.

“Tumeajiriwa wengi ni vijana na tunatokea familia tofauti ila sasa tunapata motisha na namna nzuri ya kukabiliana na mazingira tunayokutana nayo tumeelekezwa kujitambua kwamba tukiyabeba yale tuliyotoka nayo vyuoni tungeharibu,“ alisema Mwl. Lupakisyo Mwakipiti.
Naye Afisa Maendeleo Sara Muhoni amesema, “nimeweza kueleweshwa juu ya wajibu wangu kazi maana sisi ajira mpya tunaingia bila kujua majukumu yetu kazini sasa tumeelekezwa kujitambua na kujiepusha na vitendo vyote viovu kama kupokea na kutoa rusha pamoja na maadili hii ni faida kubwa kwangu.”
Mafunzo elekezi kwa watumishi wa Umma yanatolewa chini ya Waraka namba 5 wa mwaka 2011 wa Mkuu wa Utumishi wa Umma.
Discussion
Reader comments
0 contributions