Katika kuwajengea uwezo Watendaji wa Kata kuhusu Mfumo wa Kitaifa wa Anwani za Makazi na Postikodi (NaPA), Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi imeendesha mafunzo maalum katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watendaji hao namna ya kutumia mfumo wa NaPA katika kutambua, kusajili na kusimamia taarifa za anwani za makazi pamoja na postikodi katika maeneo yao. Mfumo huo ni muhimu katika kuweka utambulisho sahihi wa maeneo, nyumba na makazi ya wananchi kwa kutumia taarifa zinazoweza kutumika kwa urahisi katika utoaji wa huduma mbalimbali.
Aidha, watendaji hao wameelekezwa kuhakikisha taarifa zinazoingizwa katika mfumo zinakuwa sahihi, kamili na zinahuishwa kwa wakati, ili kuwezesha Serikali na wadau mbalimbali kupata taarifa sahihi za maeneo na makazi, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma zinazohitaji utambuzi wa anwani za wananchi.
Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi katika kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utendaji wa Serikali na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions