Na Ibrahim Rojala - Geita.
Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu mkazi Geita, watuhumiwa watatu kwa makosa manne ikiwa ni pamoja na kosa la uhujumu uchumi na kukwepa kodi zaidi ya Shilingi milioni 171.51.
Waliofikishwa mahakamani katika shauri hilo namba 11236/2026 ni Bernado Wandela (Mkurugenzi wa kiwanda cha Makha Beverage Company Limited), Batholomeo Philipo ‘Shauri’ ambaye ni mkemia na mshtakiwa wa tatu ni kiwanda cha Makha Beverage Company Limited.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo mnamo Mei 14, 2026 katika mtaa wa Magogo ‘A’, Manispaa ya Geita ambapo walikutwa na Box 451 ya Pombe kali aina ya Doz M Vodka yakiwa na Stempu za kughushi na kukwepa kodi ya Shilingi milioni 171,516,454.

Aidha Mashtaka hayo yamesomwa Ijumaa Mei 21, 2026 na mwendesha mashtaka wa Serikali Jaines Kihwelo akisaidiana na Auni Chilamula mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama Cleofas Waane.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Wakili wa Serikali Auni Chilamula,ameyataja makosa yanayowakabili kuwa ni kukutwa na bidhaa zilizowekwa stempu za kughushi ambayo ni kinyume na kanuni ya 36(1)(i) ya kanuni ya Stempu za kielektroniki ya mwaka 2018 iliyofanyiwa marekebisho ya kanuni ya 3(e) ya marekebisho ya kanuni za Stempu za kielektroniki ya mwaka 2024.

Kosa la pili ni kukwepa kodi kwa njia ya udanganyifu kinyume na kifungu cha 95(1)(d) cha Sheria ya usimamizi wa kodi,Sura ya 438 marejeo ya 2023.Kosa la tatu ni kusababisha hasara kwa Serikali kinyume na aya ya 10(1) ya jedwali la kwanza ikisomwa pamoja na (57)(1) na 61(2) ya makosa ya uhujumu uchumi sura ya 200 marejeo ya 2023.
Aidha kosa la nne ni utakatishaji fedha ambayo ni kinyume na kifungu cha 12(d) na 13(1)(a) cha Sheria ya utakatishaji fedha Sura ya 12 iliyofanyiwa marekebisho 2023.
Meneja wa upelelezi wa kodi Kanda ya Ziwa Joel Mbilinyi,amesema licha ya Mfanyabiashara huyo kusajiliwa na Mamlaka ya mapato TRA, mtuhumiwa anakabiliwa na tuhuma za kukwepa kodi ambapo amebainisha kwamba idara hiyo itaendelea kupokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema na kuwawajibisha wote wenye tabia kama hiyo.

“Mamlaka itaendelea kutoa elimu kwa walipa kodi na kwa wananchi na wadau wote,bado tunafanya ufuatiliaji hivi vitu ni vya jinai uzalishaji wake ni wa siri mno na ndiyo maana tunaihamasisha jamii kutoa taarifa za siri zinazohusiana na ukiukwaji wa taratibu za kodi”
Baada ya kusikilizwa kwa shauri hilo, watuhumiwa wamepelekwa rumande kutokana na shtaka la tatu ambalo ni la uhujumu uchumi kutokuwa na dhamana, huku uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili ukiendelea.
Discussion
Reader comments
0 contributions