Wizara ya Katiba na Sheria imewahimiza Watanzania kujenga utamaduni wa kutumia njia mbadala za utatuzi wa migogoro badala ya kukimbilia mahakamani, ikieleza kuwa mfumo huo husaidia pande zote zinazohusika kupata suluhu ya amani na kudumisha mshikamano wa jamii.
Hayo yamebainishwa Julai 1, 2026 na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainabu Katimba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria kwenye Viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) jijini Dar es Salaam.

Katimba amesema wizara hiyo imejitokeza katika maonesho hayo kwa lengo la kuwafikia wananchi moja kwa moja kwa kuwapatia huduma mbalimbali za kisheria pamoja na ushauri kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika maisha yao ya kila siku.
"Nitumie fursa hii kuwakaribisha Watanzania wote kutembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria ili kupata huduma za kisheria, ushauri pamoja na elimu kuhusu haki na wajibu wao," amesema.

Amesisitiza kuwa pamoja na mahakama kuwa na mamlaka ya kusimamia utoaji wa haki, njia mbadala za utatuzi wa migogoro zina nafasi muhimu katika kujenga maridhiano na kupunguza migogoro inayoweza kudumu kwa muda mrefu.
Katimba amesema kupitia maonesho hayo, maafisa wa wizara wanazungumza na wananchi wanaofika bandarini hapo ili kuwasaidia kutambua njia sahihi za kushughulikia migogoro yao kwa mujibu wa sheria.
Discussion
Reader comments
0 contributions