Na Clavery Christian, Bukoba - Kagera
Wataalamu 57 wa afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba wamepatiwa mafunzo maalum kuhusu namna ya kumtambua na kumhudumia mhisiwa wa ugonjwa wa Ebola, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Akitoa mafunzo hayo, Mtaalamu wa Epidemiolojia kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Philipo Lambo Shineneko, alisema utambuzi wa mhisiwa wa Ebola hufanyika kwa kuzingatia dalili maalum za kiafya pamoja na historia ya mtu husika, ikiwemo iwapo ametokea au kutembelea eneo ambalo mlipuko wa ugonjwa huo umethibitishwa kuwepo.

Dkt. Shineneko alieleza kuwa mhisiwa wa Ebola anaweza kuonyesha homa kali ya ghafla ya nyuzi joto 38 au zaidi pamoja na angalau dalili mbili kati ya maumivu makali ya kichwa, uchovu usio wa kawaida, maumivu ya misuli na viungo, kutapika, kuharisha, maumivu ya tumbo, na katika hatua za baadaye kutokwa na damu kwenye fizi, pua, macho au sehemu nyingine za mwili.
Alisisitiza kuwa si kila mtu mwenye dalili hizo huhesabika moja kwa moja kuwa na Ebola, bali mtu huchukuliwa kuwa mhisiwa pale anapokuwa na dalili hizo na wakati huohuo akiwa ametoka katika eneo lenye mlipuko wa Ebola au amewahi kutangamana na mgonjwa wa Ebola au mtu aliyefariki kutokana na ugonjwa huo.

Katika mafunzo hayo, washiriki walikumbushwa hatua muhimu za kuchukua wanapokutana na mhisiwa wa Ebola. Hatua hizo ni pamoja na kuvaa vifaa vya kujikinga kabla ya kumgusa mhisiwa, kumtenga mara moja na watu wengine, kutoa taarifa kwa mamlaka za afya kwa haraka, kuchukua taarifa zake pamoja na za waliotangamana naye katika fomu maalum, na kuhakikisha anapelekwa kwenye kituo cha afya kilichoandaliwa kushughulikia magonjwa ya mlipuko.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba, Dkt. Museleta Nyakiroto, alimshukuru Dkt. Shineneko na Wizara ya Afya kwa kuendelea kupeleka wataalamu hospitalini hapo kwa ajili ya kujengeana uwezo kuhusu magonjwa ya mlipuko.
Aidha, aliwataka watumishi waliopatiwa mafunzo hayo kuyatumia ipasavyo katika maeneo yao ya kazi ili kuimarisha utayari wa hospitali na jamii katika kukabiliana na hatari ya magonjwa ya mlipuko kama Ebola.


Discussion
Reader comments
0 contributions