Na William Bundala, Kahama - Shinyanga.
Umoja wa wastaafu Tanzania (REAT), wameiomba serikali kuingizwa kwenye bodi za mifuko ya hifadhi ya jamii ili kutetea maslahi yao.
Ombi hilo limetolewa na rais wa wastaafu Tanzania Mohamed Bilikesi wakati wa mkutano wa wastaafu uliofanyika wilayani Kahama ukijumuisha wastaafu wa halmashauri ya Ushetu,Kahama Manispaa na Halmashauri ya Msalala.

Bilikesi amesema kuwa wastaafu wengi wanakosa haki zao kutokana na kutokuwa na mtu wa kuwasemea katika ngazi za juu za maamuzi zikiwemo bodi za mifuko ya jamii.
“Tunaiomba serikali wastaafu tuingizwe katika bodi za mifuko ya hifadhi ya jamii ili nasi tuwe na watetezi katika kufanya maamuzi,mana kuna haki nyingi za wastaafu hazizingatiwi na matokeo yake wengi wanafariki bila kupata stahiki zao za msingi,” amesema Bilikesi.

Katika hatua nyingine Bilikesi ametoa wito kwa wastaafu wote nchini kuzingatia afya zao a kuhakikisha hawajiingizi katika biashara ngumu ambazo hawajawahi kuzifanya kwani zitawapa changamoto nyingi na kupata msongo wa Mawazo.
“Niwaombe wastaafu wenzangu kwanza hakikisheni mnazingatia afya zenu pia epukeni kujiingiza katika biashara ambazo hamna uzoefu nazo,mkijiingiza katika iashara msizokuwa na uwezo nazo zitawapa changamoto na matokeo yake mtapata msongo wa Mawazo,” smesisitiza Bilikesi.

Nao baadhi ya wastaafu walioshiriki kikao hicho wameshukuru kuanzishwa kwa taasisi hiyo kwani itawasaidia kufikisha kero zao hasa za mapunjo ya mishahara na gharama za kusafirisha mwili wa mstaafu na familia yake Kwenda nyumani kwao alikozaliwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya mawasiliano kwa wastaafu Tanzania, Tabu Mambo ameiomba serikali kupitia benki kuu kupunguza riba za mikopo kwa wastaafu katika taasisi za kibenki kwakuwa kipato chao hakilingani na wafanyakazi waliopo makazini.

“Ombi letu kwa serikali kupitia benki kuu,tunaomba sana riba za mikopo zipungue kwa wastaafu kwenye taasisi za kibenki,kipato chetu ni tofauti na watumishi ambao wapo kazini,tukipunguziwa riba itatusaidia kukopa na kulipa kwa wakati ili tuweze kujikimu katika maisha yetu,” amesema Bi Mambo.
“Tunashukuru sana kwakweli kuanzishwa kwa taasisi hii,tumesumuka sana kufikisha malalamiko yetu ngazi za juu za maamuzi,ni matumaini yetu kuwa tumepata chombo cha kutusemea kwakuwa wapo wazee wengine hawawezi hata Kwenda sehemu wakasimama kwa muda mrefu na kutoa matatizo yao,” Wamesema wastaafu hao.

Discussion
Reader comments
0 contributions