Na Adam Msafiri - Mara.
Wasichana na Wanafunzi Wilayani Serengeti mkoani Mara, wamehimizwa kutambua, kulinda na kutetea haki zao, huku wakikumbushwa kuwa ukimya dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia unachangia kuwanyima fursa ya kutimiza ndoto zao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Wito huo umetolewa wakati wa kongamano la elimu lililowakutanisha zaidi ya wasichana 300 kutoka Shule za Sekondari Mariwanda na Chief Salota, lililolenga kuwajengea uelewa kuhusu haki za mtoto wa kike, kupinga ukatili wa kijinsia na kuhamasisha mapambano dhidi ya mila na desturi zinazokiuka haki za wanawake na watoto.

Washiriki wa kongamano hilo wameeleza kuwa vitendo vya ukeketaji, ndoa za utotoni na aina nyingine za ukatili wa kijinsia vinaendelea kuwanyima wasichana wengi haki ya kupata elimu na kutimiza ndoto zao. Wameitaka Serikali pamoja na wadau wa maendeleo kuhakikisha sheria zilizopo zinatekelezwa kikamilifu na wahusika wa vitendo hivyo wanachukuliwa hatua kali za kisheria.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki kongamano hilo, akiwemo Ada Ryoba, Fatuma Ramadhani na Magori Sobela, wamesema elimu waliyoipata imewajengea ujasiri wa kutambua haki zao na kutoa taarifa wanapokumbana na vitendo vya ukatili badala ya kuvifumbia macho.

Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Shirika la Grumeti Fund, Elizabeth Magoto, amesema taasisi hiyo imeendelea kuwekeza katika programu zinazowawezesha watoto wa kike kuendelea na masomo, kujenga kujiamini na kuwa na uwezo wa kupaza sauti wanapokiukwa haki zao.
Naye Afisa Rasilimali Watu wa Grumeti Fund, Amsi Nyambuche, amesema vita dhidi ya ukatili wa kijinsia haviwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa wazazi, viongozi wa jamii, Serikali na wadau mbalimbali.

Amesisitiza kuwa kila mtoto wa kike anapaswa kupewa mazingira salama ya kujifunza, kukua na kutimiza ndoto zake bila kukumbwa na vitendo vya ukatili au mila zinazomnyima haki zake za msingi.
Kongamano hilo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuimarisha ulinzi wa mtoto wa kike na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kutokomeza ukatili wa kijinsia ili kujenga kizazi chenye usawa, elimu na fursa sawa kwa wote.
Discussion
Reader comments
0 contributions