Na Gideon Gregory - Dodoma.
Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana leo Juni 5,2026 imetangaza rasmi orodha ya washiriki 100 waliofanikiwa kuingia hatua inayofuata ya Shindano la Vijana Uchumi Challenge 2026, baada ya mchakato ulioshirikisha maombi 7,852 kutoka mikoa yote nchini kukamilika.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, leo Juni 05,2026 Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge, Amina Sanga, amesema mwitikio wa vijana waliojitokeza kushiriki unaonesha namna wanavyotambua nafasi yao katika kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa kupitia mawazo bunifu na yenye tija.
Bi. Sanga amebainisha kuwa kati ya maombi yote yaliyopokelewa, maombi 4,121 sawa na asilimia 52.5 yamekidhi vigezo vya msingi vilivyowekwa, huku mawazo 458 yakifanikiwa kupata alama za juu na kuwasilishwa katika hatua ya mwisho ya uchambuzi kabla ya kupatikana kwa washiriki 100 bora.

“Tunapenda kusisitiza kuwa kufika katika kundi la washiriki 100 bora ni mafanikio makubwa kwani kulikuwa na ushindani mkubwa na washiriki wamechaguliwa kwa kuzingatia ubora wa mawazo yao, ubunifu na athari zake katika uchumi wa Taifa,” amesema.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, sekta ya TEHAMA na huduma za kidigitali inaongoza kwa asilimia 30.7 ya mawazo yote yaliyowasilishwa, ikifuatiwa na Kilimo na Teknolojia za Kilimo kwa asilimia 27.8, huku sekta ya Viwanda na Uzalishaji ikichangia asilimia 21.3.
Washiriki 100 waliochaguliwa sasa wanatarajiwa kushiriki kambi maalum ya siku Nne itakayowapa mafunzo ya kitaalamu, ushauri wa kuboresha mawazo yao pamoja na mbinu za kufanya mawasilisho yenye ushawishi mbele ya majaji, wawekezaji na wadau wa maendeleo.

Katika hatua nyingine, amesema kuongezwa kwa zawadi za shindano hilo kufuatia mwitikio mkubwa wa vijana na ubora wa mawazo yaliyowasilishwa. Mshindi wa kwanza sasa atajishindia Sh milioni 50 badala ya Sh milioni 30 zilizokuwa zimetangazwa awali.
“Mshindi wa kwanza atajinyakulia kiasi cha shilingi milioni 50, mshindi wa pili milioni 30 na mshindi wa tatu milioni 20, huku washiriki wa nafasi ya nne hadi ya kumi wakipata shilingi milioni tatu kila mmoja,” anasema Sanga.
Mbali na zawadi hizo za fedha, washiriki wote 100 bora watapatiwa vyeti vya utambuzi na fursa mbalimbali za mafunzo, ushauri wa kitaalamu na kuunganishwa na taasisi zinazoweza kusaidia utekelezaji wa mawazo yao, hatua inayotarajiwa kuongeza mchango wa vijana katika kukuza uchumi wa Tanzania.
Discussion
Reader comments
0 contributions