Na Daniel Gahu - Katavi.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Hozza Mrindoko, amekemea vikali vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi na kudhuru wengine kutokana na taarifa zisizo na ukweli, akisisitiza kuwa vitendo vya aina hiyo, pamoja na kueneza uzushi, havitavumiliwa na Serikali.
Ametoa kauli hiyo mara baada ya kushiriki ibada ya Pasaka katika Kanisa la Anglikana lililopo Kata ya Makanyagio, Manispaa ya Mpanda ambapo amesema baadhi ya taarifa zinazosambazwa mitandaoni na katika jamii, hususan zile zenye mwelekeo wa kishirikina na uzushi, zimekuwa zikichochea taharuki, hofu na migogoro isiyo ya lazima.

“Wananchi wanapaswa kupuuza taarifa zisizo na uthibitisho na kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kutokana na uzushi. Serikali ipo imara na inafuatilia kwa karibu masuala yote yanayoendelea,” amesema Mrindoko.
Ameongeza kuwa vyombo vya dola vitaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria wote watakaobainika kuhusika katika uenezaji wa taarifa za upotoshaji na uzushi unaosababisha hofu na kuvuruga utulivu wa jamii.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama katika Mkoa wa Katavi ni shwari, na kuwataka kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu yoyote.
Katika hatua nyingine, amewahimiza waumini na wananchi kwa ujumla kuendeleza moyo wa upendo, mshikamano na kusaidiana, hasa kwa makundi yenye uhitaji, sambamba na kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki cha maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka.



Discussion
Reader comments
0 contributions