Na Clavery Christian, Karagwe - Kagera.
Baadhi ya wananchi waliokuwa wakisumbuliwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho kwa muda mrefu wameelezea furaha yao baada ya kurejeshewa uwezo wa kuona kufuatia kufanyiwa upasuaji katika kambi maalum ya huduma za macho inayoendelea katika Kituo cha Afya Kayanga, Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.
Miongoni mwa wanufaika wa huduma hiyo Bi. Adaraida Joseph, mkazi wa Kijiji cha Mugaba wilayani Karagwe, alisema kabla ya kufanyiwa upasuaji alikuwa amepoteza uwezo wa kuona kiasi cha kushindwa kujitegemea na kutegemea msaada wa watu wengine katika shughuli zake za kila siku.
Amesema maisha yake yalikuwa magumu kutokana na kutoweza kuona hata watu waliokuwa karibu naye, hali iliyomlazimu kushikwa mkono kila alipokuwa akihitaji kusafiri au kutekeleza shughuli mbalimbali.

“Niliteseka sana, sikuwa namtambua mtu yeyote, nilikuwa nasikia sauti tu. Hata nilipokuja hapa nililetwa kwa kushikwa mkono. Lakini sasa naona vizuri, hata nikirudi nyumbani sitashikwa mkono tena kwa sababu naona,” alisema Bi, Aderaida.
Naye George Venance ameishukuru Serikali, Shirika la KCCO pamoja na madaktari bingwa wa macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Bukoba, kwa kuandaa huduma hiyo ambayo alisema imewarejeshea matumaini na furaha wananchi wengi waliokuwa wameathirika na matatizo ya macho.
Aliwahimiza wananchi wengine wenye changamoto za macho kujitokeza kwa wingi kila wanaposikia taarifa za uwepo wa kambi za uchunguzi na matibabu, ili waweze kupata huduma mapema na kuepuka madhara makubwa zaidi.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya kambi hiyo, Daktari Bingwa wa Macho, Dkt. Daniel Mashamba, alisema kuwa katika siku ya jana wagonjwa 19 walifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho na wote wanaendelea vizuri baada ya matibabu hayo.
Alieleza kuwa wagonjwa hao waliruhusiwa kurejea nyumbani baada ya madaktari kujiridhisha na hali zao za kiafya na maendeleo mazuri ya macho yao baada ya upasuaji.
Kambi hiyo imeendelea kuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Karagwe na maeneo jirani kwa kuwapatia huduma za kibingwa ambazo zimechangia kurejesha uwezo wa kuona kwa wagonjwa wengi na kuboresha maisha yao ya kila siku.
Discussion
Reader comments
0 contributions