Na Clavery Christian, Bukoba - Kagera.
Mkoa wa Kagera umeendelea kukabiliwa na changamoto ya ushiriki mdogo wa wanawake na vijana katika vyama vya ushirika, hali inayotajwa kuchangia kuendelea kwa biashara ya mazao nje ya mfumo rasmi na kuathiri ubora wa kahawa pamoja na mapato ya wakulima.
Hayo yalielezwa katika Jukwaa la Nne la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Kagera, ambapo viongozi wa sekta ya ushirika walijadili mafanikio na changamoto zinazoikabili sekta hiyo katika kuimarisha uchumi wa wakulima.

Akizungumza katika jukwaa hilo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Kagera, Golieth Elias, alisema kuwa licha ya vyama vya ushirika kuwa na wanachama zaidi ya 109,000, bado idadi ya wanawake na vijana wanaojiunga na vyama hivyo ni ndogo, hali inayochangia baadhi ya wakulima kuuza mazao yao nje ya mfumo wa mnada rasmi, jambo linalochochea uuzaji wa kahawa mbichi na kupunguza ubora wa zao hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahaya Kido, amesema ushirika una nafasi kubwa katika kuwaunganisha wakulima, wafugaji na wavuvi ili kuongeza tija na mapato. Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa mazao na kudhibiti utoroshaji wa kahawa, akibainisha kuwa hatua hiyo itawawezesha wakulima kupata manufaa zaidi kutokana na jasho lao.

Naye Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania Bara, Benson Ndiege, alitoa wito kwa vyama vya ushirika kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usajili wa wanachama na usimamizi wa taarifa mbalimbali pamoja na matumizi ya teknolojia yatakayoongeza uwazi, ufanisi na kuimarisha utoaji wa huduma katika sekta ya ushirika nchini.
Viongozi hao kwa pamoja walihimiza wanawake na vijana kujitokeza kwa wingi kujiunga na vyama vya ushirika ili kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na sekta hiyo na kuchangia maendeleo ya jamii pamoja na taifa kwa ujumla.
Discussion
Reader comments
0 contributions