Skip to main content

WANANCHI WAONGEZE AKIBA YA CHAKULA KWA TAIFA - NFRA SHINYANGA

Na Thobias Mwanakatwe, Nzega - Tabora.

WANANCHI WAONGEZE AKIBA YA CHAKULA KWA TAIFA - NFRA SHINYANGA
Studio Narration JAMBO FM

WANANCHI WAONGEZE AKIBA YA CHAKULA KWA TAIFA - NFRA SHINYANG...

0:00 --:--

Na Thobias Mwanakatwe, Nzega - Tabora.

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Kanda ya Shinyanga, umewataka wakulima na wananchi kuendelea kuuza mazao yao kwa wakala huo ili kuimarisha akiba ya chakula ya taifa na kuhakikisha nchi inakuwa na chakula cha kutosha wakati wote, hususan nyakati zinazoweza kujitokeza changamoto za upatikanaji wa chakula.

Wakala huo umesema ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga hifadhi imara ya chakula nchini, itakayosaidia kukabiliana na hali ya upungufu wa chakula inayoweza kusababishwa na sababu mbalimbali, ikiwamo mabadiliko ya tabianchi, ukame na mvua zisizotabirika.

Meneja wa NFRA Kanda ya Shinyanga, Dickson Nyika, alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea eneo la ujenzi wa ghala la kuhifadhi nafaka linalojengwa katika Kijiji cha Itilo, Wilaya ya Nzega, Mkoa wa Tabora, akisisitiza kuwa wakulima wanapaswa kuona umuhimu wa kuuza mazao yao kwa wakala huo kwa kuwa wana mchango wa moja kwa moja katika kuhakikisha taifa linakuwa na chakula cha kutosha.

Nyika alisema wananchi wanapouza mazao yao kwa NFRA hawachangii tu kukuza uchumi na kuongeza kipato cha familia zao, bali pia wanatekeleza jukumu muhimu la kitaifa la kuweka akiba ya chakula kitakachoweza kutumika wakati wa dharura.

Alisema ni muhimu kwa wakulima kuelewa kuwa mazao wanayouza kwa NFRA yanakuwa sehemu ya akiba ya chakula ya taifa, ambayo baadaye inaweza kurejeshwa sokoni wakati wa upungufu wa chakula ili kuwawezesha wananchi kupata bidhaa hiyo kwa bei wanazoweza kumudu.

“Wananchi wanapaswa kutambua kuwa wanapoiuzia NFRA nafaka zao, wanakuwa wamechangia kuweka akiba ya taifa ambayo kimsingi ni kwa ajili yao wenyewe. Hivyo, tunawaomba waendelee kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha tunakuwa na chakula cha kutosha,” alisema Nyika.

Alisema katika msimu wa ununuzi wa mwaka huu, wakala huo unaendelea kununua nafaka kutoka kwa wananchi licha ya kukabiliwa na changamoto ya ushindani wa bei unaotokana na wafanyabiashara binafsi kupandisha bei za mazao, hali inayoweza kuwafanya baadhi ya wakulima kuvutiwa zaidi na kuuza kwa wafanyabiashara hao.

Hata hivyo, alisema NFRA inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kuuza mazao yao kwa wakala huo, akieleza kuwa tofauti kubwa kati ya kuuza kwa NFRA na wafanyabiashara binafsi ni kwamba mazao yanayonunuliwa na wakala huo huhifadhiwa kwa matumizi ya baadaye, hasa wakati wa dharura.

Alifafanua kuwa pale taifa linapokuwa na chakula cha kutosha, NFRA huendelea kukihifadhi, lakini endapo kutatokea upungufu unaosababisha bei kupanda sokoni, wakala huo unaweza kuingilia kati kwa kuuza chakula kilichohifadhiwa ili kuongeza upatikanaji na kupunguza athari za kupanda kwa bei kwa wananchi.

“Unapoiuzia NFRA nafaka zako, unakuwa na uhakika kuwa chakula hicho kinahifadhiwa. Ikifika kipindi ambacho kutakuwa na uhitaji mkubwa, kama vile kinapotokea kipindi cha El Niño na upatikanaji wa chakula kuwa mgumu, chakula tulichonunua kutoka kwa wananchi kinaweza kuuzwa tena kwa bei wanayoweza kumudu,” alisema.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda wananchi dhidi ya athari za wafanyabiashara kupandisha bei za vyakula wakati uzalishaji unapokuwa mdogo au upatikanaji wake unapokuwa mgumu.

Nyika alisema NFRA ina jukumu la kusaidia kuhakikisha chakula kinapatikana kwa wananchi kwa bei inayokubalika, hasa katika kipindi ambacho soko linakuwa na changamoto ya upatikanaji wa nafaka.

Alisema wakala huo unapotambua kuwa kuna changamoto ya upatikanaji wa chakula au kupanda kwa bei kutokana na upungufu wa bidhaa hiyo, unaweza kuingilia soko kwa kutoa chakula kilichohifadhiwa ili kusaidia kuongeza upatikanaji wake.

Aidha, aliwataka wananchi kuwa na utaratibu mzuri wa kusimamia mazao wanayovuna, akisisitiza kuwa si busara kuuza chakula chote mara baada ya mavuno bila kuacha kiasi cha kutosha kwa ajili ya matumizi ya familia zao.

“Nawasihi wananchi wasiuze chakula chote walichovuna. Ni muhimu waweke akiba kwa ajili ya matumizi ya familia zao, lakini pia wafahamu kuwa wanapoiuzia NFRA wanakuwa wamechangia kujenga akiba ya taifa ambayo ni kwa manufaa yao wenyewe,” alisema.

Katika hatua nyingine, Nyika alisema ujenzi wa ghala jipya la kuhifadhi nafaka katika Kijiji cha Itilo, Wilaya ya Nzega, utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora na maeneo jirani, kutokana na uwezo wake wa kuhifadhi tani 10,000 za nafaka.

Alisema kukamilika kwa ghala hilo kutarahisisha upatikanaji wa chakula katika eneo hilo wakati wa mahitaji, badala ya kutegemea chakula kinachosafirishwa kutoka mikoa mingine kama Shinyanga na Musoma.

“Kwa mfano, katika Mkoa wa Tabora, tukiweza kujaza ghala hili lenye uwezo wa kuhifadhi tani 10,000, kutakapokuwa na uhaba wa chakula itakuwa rahisi kuwafikia wananchi. Hakutakuwa na ulazima wa kusafirisha chakula kutoka Shinyanga au Musoma kwa sababu kitakuwa kimehifadhiwa hapa hapa,” alisema.

Alisema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu ya hifadhi ya chakula nchini, kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka katika maeneo mbalimbali na kuhakikisha chakula kinapatikana karibu na wananchi wanaokihitaji.

Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, NFRA na wakulima ni nguzo muhimu katika kuhakikisha taifa linakuwa na usalama wa chakula, huku akiwataka wananchi kutumia fursa ya kuuza mazao yao kwa wakala huo na wakati huohuo kuzingatia umuhimu wa kubakiza chakula cha kutosha kwa matumizi ya familia zao.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.