Skip to main content

WANANCHI WAHIMIZWA KUTUNZA MAZINGIRA, VYANZO VYA MAJI

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

WANANCHI WAHIMIZWA KUTUNZA MAZINGIRA, VYANZO VYA MAJI

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Shirika la Tanganyika Christian Refugee Service (TCRS), kwa ufadhili wa kifedha kutoka Shirika la Norwegian Church Aid (NCA), limefanikisha kwa mafanikio makubwa kupandwa kwa miche Zaidi ya miatatu hamsini ya matunda  vivuli na mbao   pamoja na miche  mia tano  kugawiwa kwa wananchi katika kata ya Maganzo halimashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga  ili kuhamasisha utunzaji wa mazingira, upandaji miti na usafi wa maeneo ya huduma za jamii.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Afisa Tarafa wa Kishapu, Fadhili Mvanga, amepongeza TCRS na NCA kwa kuendelea kuwekeza katika shughuli za maendeleo ya jamii hususan uhifadhi wa mazingira na kuanisha kuwa wadau wa maendeleo wamekuwa nguzo muhimu katika kuibua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi na kushirikiana na serikali katika kuzitafutia ufumbuzi endelevu.

"Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na TCRS pamoja na Norwegian Church Aid katika kuhamasisha jamii kutunza mazingira. Haya si maadhimisho ya siku moja pekee bali ni mwanzo wa dhamira ya kudumu ya kuhakikisha tunarithisha kizazi kijacho mazingira salama na yenye uhai. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kupanda miti, kuitunza na kulinda rasilimali za asili kwa manufaa ya Taifa letu," amesema Mvanga.

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika kampeni za upandaji miti na usafi wa mazingira huku akisisitiza kuwa maendeleo ya kiuchumi hayawezi kupatikana bila kuwa na mazingira bora na salama.



Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Maganzo,  Hamza Tandiko, amesema viongozi wa kata hiyo wanaendelea kusimamia kwa karibu shughuli za utunzaji wa mazingira na upandaji miti ili kuhakikisha maeneo yote yanakuwa ya kijani na yenye kuvutia na kuongeza kuwa  upatikanaji wa maji kutoka Ziwa Victoria umeongeza fursa ya wananchi kupanda na kutunza miti kwa urahisi zaidi.


"Tunatoa wito kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuendelea kutupatia miche ya kutosha ya miti. Pia wananchi watumie fursa zilizopo ikiwemo kupata miche katika maeneo mbalimbali kama Mwadui ili kuhakikisha kila kaya inapanda miti. Tunahitaji Maganzo na Kishapu kwa ujumla kuwa mfano wa utunzaji wa mazingira nchini," amesema Tandiko.



Naye Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Cassim Said, amesema Halmashauri imeendelea kuweka sera, mikakati na mipango mbalimbali ya kuhakikisha mazingira yanatunzwa na sheria zote za mazingira zinatekelezwa ipasavyo.


Amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuhamasisha upandaji miti katika taasisi za umma, shule, vituo vya afya na makazi ya wananchi pamoja na kuimarisha elimu ya mazingira kwa jamii.



"Halmashauri itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mazingira kwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu sahihi kuhusu uhifadhi wa mazingira. Tunataka kuona kila mwananchi anakuwa mshiriki wa moja kwa moja katika kulinda mazingira kwa kupanda miti, kuzuia uharibifu wa vyanzo vya maji na kusimamia usafi katika maeneo yao," amesema Cassim Said.

Akizungumza kwa niaba ya TCRS Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Sanyenge, amesema shirika hilo linaamini kuwa maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila uwepo wa mazingira bora, na kuanisha kuwa TCRS imeendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine katika kutekeleza miradi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi kupitia uhifadhi wa mazingira ,usimamizi wa rasilimali za asili na uhamasishaji wa jamii.



"Tunajivunia kuona wananchi wa Kishapu wanaitikia kwa vitendo wito wa kutunza mazingira. Kupitia ufadhili wa Norwegian Church Aid, tumeweza kufanikisha shughuli hizi ambazo zina mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ustawi wa jamii. Tutaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho," amesema Sanyenge.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Norwegian Church Aid (NCA), Emmanuel Temu, amesema taasisi hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na mashirika ya maendeleo katika kulinda mazingira kwa kuwa ni msingi wa maisha na maendeleo ya wananchi.
"Mazingira ni urithi wetu wa pamoja. Norwegian Church Aid inaamini kuwa uwekezaji katika uhifadhi wa mazingira ni uwekezaji katika afya, uchumi na ustawi wa jamii. Tunaendelea kushirikiana na TCRS kwa sababu tunaona matokeo chanya yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja," amesema Temu.



Nao baadhi ya wananchi walioshiriki zoezi hilo akiwemo Costantine Weja  mkazi wa  Kijiji cha Bulima, Kata ya Idukilo, na Valentina Gayagamba mkazi wa kata ya Maganzo wamesema utunzzaji wa mazingira ni suala la lazima katika jamii kwani  wameshuhudia manufaa makubwa yatokanayo na utunzaji wa mazingira na upandaji miti ikiwemo kuboreka kwa hali ya hewa na kuongezeka kwa kivuli katika maeneo mbalimbali ya makazi.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.