Na Ibrahim Rojala - Geita.
Wakazi wa kitongoji cha Bujingwa kata ya Nyanguku, Halmashauri ya Manispaa ya Geita wameiomba serikali kuingilia kati na kukamilisha mradi wa kisima cha maji ambao utekelezaji wake umekwama kwa kipindi cha miaka minne tangu kisima hicho kilipochimbwa mnamo mwaka 2022.
Wakizungumza kuhusiana na changamoto hiyo wakiwa katika eneo ambalo kisima hicho kilichimbwa tangu mwaka 2022 na Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Geita (GEUWASA),wamesema hivi sasa wamekuwa wakisumbuka mno kupata huduma ya maji kwa kutembea umbali mrefu kufuata maji katika vitongoji vingine.

"Tuna miaka minne tunasubiria maji, hamtengenezi, kwahiyo tunaomba mtusaidie sana katika hilo," amesema Monica Lucas.
Naye Mohamed Masele Kipili amasema tangu kuanza kwa Mradi huo katika kipindi cha miaka minne iliyopita umeshindwa kukamilika hali inayowafanya kuanza kukosa imani na serikali pamoja na chama chao kuhusiana na mradi husika ambao hadi sasa umegharimu kiasi cha shilingi milioni 200.

Wakizungumzia adha changamoto zinazojitokeza ndani ya ndoa na familia kwa ujumla zinazosababishwa na kukosekana kwa huduma ya maji ), Bi.Winifrida John amesema ndoa zimekuwa zikikabiliwa na changamoto kutokana na kukosekana kwa huduma ya maji, hoja iliyoungwa mkono na Bi. Rosemary Bahati Shigela ameeleza kuwa wamekuwa wakitumia muda mrefu kutafuta maji hivyo kushindwa kutimiza majukumu mengine ya kifamilia, ikiwemo faragha ya ndoa.

"Muda mwingine inachochea yaani kutokupata watoto kwasababu yaani ule muda ukifika mwanaume akikwambia kwamba nahitaji hiki na hiki huwezi,unakuwa mkali,kwasababu ya maji," ameeleza Rosemary
Mmoja kati ya wazee wa Kitongoji hicho, Shadrack Mashamba ameeleza kuwa utafiti wa Mradi huo ulianza mwezi wa tano mwaka 2022 ukihusisha maeneo matatu,mwezi wa nane mwaka huo zoezi la uchimbaji lilianza na kukamilika Agosti 11, 2022 mwaka na kuelezea kwamba walikuwa na matumaini kwamba utakamilika ndani ya muda mfupi tofauti na hali ilivyo sasa.

Ameiomba serikali kupitia wizara ya maji kukamilisha Mradi huo ambao unategemewa pia na maeneo yanayotoa huduma za kijamii kama vile maeneo ya huduma za afya na shule zilizopo ndani ya kata ya Nyanguku.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nyanguku, Fitina Mageleja Bufumbe amekiri uwepo wa changamoto hiyo na kueleza kwamba Mradi huo haujakamilika kama ilivyokuwa imeahidiwa na wakandarasi na kueleza kwamba wananchi wamekuwa wakifuata maji katika vitongoji vingine na kuomba serikali kukamilisha mradio huo ili wananchi waweze kupata maji kutoka katika Mradi huo unaoelezwa kuwa umegahrimu kiasi cha shilingi milioni 200.

"Ni wakazi 3700 na kitu hivi waliotakiwa wanufaike na haya maji,kwaufupi Nyanguku hatuna kisima ambacho kinaweza kikawalinda moja kwa moja wananchi cha bomba hatuna,tulikuwa tunaomba serikali ifanye juu chini huu Mradi ukamilike kwa wakati ingawaje uko nje ya wakati lakini tulikuwa tunaomba serikali juu chini sasa ili wnanchi wayapate haya maji kwa muda muafaka," amesema Fitina.
Mnamo Mei 7, 2026, Diwani wa Kata ya Nyanguku ambayepia ni Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Geita, Elias Ngole alielezea changamoto hiyo akisema kumekuwa na mkanganyiko wa maelezo kutoka kwa watekelezaji wa Mradi huo (GEUWASA).

Amebainisha kuwa awali ilielezwa kwamba sola zipo na kinachosubiriwa ni malipo ya mkandarasi ili kukamilisha Mradi huo,kabla ya maelezo yaliyotolewa na Mhandisi Yohana Masheria Mei 07,2026 yakieleza kwamba wameandikia wizarani ili kisima hicho kiweze kupatiwa fedha.
Akijibu hoja hiyo kupitia kikao hicho, Mhandisi Yohana Masheria kutoka Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira(GEUWASA) alieleza kwamba kisima hicho ni miongoni mwa visima vitano vya wabunge vilivyotolewa na kueleza kwamba kinachosubiriwa ni kukamilishwa kwa malipo ya fedhaza wakandarasi na wasambazaji wa vifaa.

Kufuatia uwepo wa changamoto hiyo,akizungumza kwa njia ya simu, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA) Mhandisi Frank Changawa amesema kuwa kisima hicho ni miongoni mwa visima vitano walivyopewa wabunge na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na kubainisha kuwa kazi katika visima vyote zinatarajiwa kuendelea kufanyika ndani ya mwezi huu wa tano na kufafanua kuwa visima hivyo vitakamilika kabla ya mwezi wa sita mwaka huu.
Discussion
Reader comments
0 contributions