Wananchi wa Kata ya Mtamaa na maeneo jirani Manispaa ya Singida Mkoani Singida wameipongeza Serikali kwa kuendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, huku wakiiomba kuendeleza huduma za madaktari bingwa katika maeneo yao ili waweze kupata matibabu bora bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda mjini.
Wananchi hao wamebainisha hayo kufuatia huduma za kibingwa zinazotolewa kwa siku tatu mfululizo katika Kituo cha Afya Mtisi, kupitia ushirikiano wa madaktari kutoka Vituo vya Afya Sokoine na Mtisi, kwa lengo la kuwafikia wananchi wanaohitaji huduma hizo.
Mkazi wa Mtisi, Nkhangaa Gawe Dule, amesema ameridhishwa na huduma alizopata kituoni hapo, akieleza kuwa alihudumiwa vizuri na kurejea kwa ajili ya kuchukua dawa. Amesema huduma hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi, hasa kutokana na gharama za nauli wanazotumia wanaposafiri kwenda mjini kutafuta matibabu.
“Nilifika hapa jana kupata huduma na nilipokelewa vizuri. Nimehudumiwa na leo nimerudi kuchukua dawa nilikuwa sitembei ila sasa natembe. Naomba Serikali iendelee kutuletea huduma kama hizi karibu na maeneo yetu kwa sababu kwenda mjini ni mbali na tunatumia nauli kubwa,” amesema Dule.
Kwa upande wake, Daud Ibrahimu, mkazi wa Kijiji cha Minyuge, Wilaya ya Ikungi, amesema alisafiri hadi Kituo cha Afya Mtisi baada ya kupata taarifa kuhusu uwepo wa madaktari bingwa waliokuwa wakitoa huduma, akieleza kuwa ameridhishwa na matibabu aliyopata.
Ibrahimu, mwenye umri wa miaka 63, amesema licha ya umbali aliotembea kutoka Minyuge hadi Mtisi, amefurahishwa na huduma alizopata na kurejea kituoni hapo kufuata dawa baada ya kuanza matibabu siku iliyotangulia.
Wananchi hao wameeleza kuwa kuendelea kusogeza huduma za madaktari bingwa katika vituo vya afya vilivyo karibu nao kutapunguza adha ya kusafiri umbali mrefu na gharama za usafiri, huku kukiwawezesha kupata huduma za matibabu kwa urahisi zaidi.

Discussion
Reader comments
0 contributions